• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mfungwa aonja uhuru kwa msamaha wa rais

Mfungwa aonja uhuru kwa msamaha wa rais

Na PHILIP MUYANGA

BAADA ya kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka 10 akitumikia kifungo kisichokuwa na mwisho kwa hatia ya kumuua mkewe na mjomba wake, Bw Peter King’ori Gitahi alipata afueni baada ya kuachiliwa huru.

Mwaka wa 2008, Bw Gitahi alipatikana na hatia ya mauaji dhidi ya mkewe Bi Nancy Nduta na mjombake William Wangombe mnamo Januari 28 mwaka wa 2008 katika eneo la Momoi,iliyokuwa wilaya ya Nakuru,lakini alikuwa na tatizo la kiakili.

Amekuwa akitumikia kifungo hicho gerezani lakini kwa mapenzi ya Rais jambo lililomfanya kuweka kesi ya kikatiba akilalamikia kukiukwa kwa haki zake.

Bw Gitahi alisema kuwa kutumikia kifungo kisichokuwa na mwisho ilikuwa ni kinyume cha haki zake za kikatiba na alitaja kifungo hicho kama chenye kudhalalisha ubinadamu.

Akimwachilia huru Bw Gitahi, Jaji Eric Ogola alisema kuwa Bw Gitahi hawezi kutumikia kifungo kisichokuwa na mwisho na kwamba alikuwa ashapona matatizo ya kiakili.

“Mahakama hii inapata ya kuwa haki za mweka kesi (Bw Gitahi) zimekiukwa wakati alipohukumiwa kutumikia kifungo kisichojulikana na kisichokuwa na mwisho,” alisema jaji Ogola.

Jaji Ogola alifunga Bw Gitahi miaka kumi na minne gerezani hesabu ikianziwa tangu Novemba 14 2008 alipowekwa gerezani lakini alisema kuwa atatumikia miaka iliyobakia nje ya jela na atakuwa chini ya afisa wa probesheni.

“Mweka kesi atakuwa akiripoti kwa chifu eneo la Lower Subukia kila tarehe kumi na tano kila mwezi kwa miezi sita kuanzia April 15 mwaka huu,” alisema jaji Ogola.

Jaji Ogola alisema kuwa kumfunga Bw Gitahi kwa muda usiojulikana kulikuwa ni kukiuka haki zake chini ya katiba.

Mahakama pia ilisema kuwa wakati bw Gitahi alikuwa hana akili timamu,inaweza kusemekana ya kuwa alikuwa hajui ni nini kilikuwa kinaendelea na ingawa alikuwa gerezani angeweza kulalamika tu kupitia kwa watu walioelewa hali yake.

“Baada ya mweka kesi kupona mwaka wa 2010 na kuwa kisheria anajua alikuwa anatumikia kifungo kisichokuwa na mwisho,alipata tabu ya kiakili (mental torture) na kudhalalishwa kibinadamu mambo ambayo katiba inatibu,”alisema Jaji Ogola.

Kulingana na ripoti ya afisa wa probesheni iliyowasilishwa mahakama,familia ya Gitahi ilikuwa tayari kumkaribisha nyumbani kwao subukia.

Jaji Ogola alisema kuwa hakukuwa na chuki yoyote na vitisho dhidi ya Bw Gitahi au kwa mtu yeytoe katika kijiji na kwamba mazingira ya nyumbani yatakuwa mwafaka kwake kurekebika.

  • Tags

You can share this post!

Finland kusaidia Kilifi kukomesha dhuluma

Wauzaji Kongowea walia kutatizwa na genge

adminleo