• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Mgeni hatarini kupoteza mali kutooa Mkenya

Mgeni hatarini kupoteza mali kutooa Mkenya

Na BRIAN OCHARO

RAIA wa Uingereza huenda akapoteza mali ya thamani ya zaidi ya Sh10 milioni kwa kukosa kumuoa mchumba wake Mkenya, ambaye sasa anaichukulia mali hiyo kama zawadi na msamaha kwa kukosa kuoana.

Bi Catherine Nduku Muema anasema mali hiyo sasa ni yake kufuatia ndoa iliyofeli na Bw Linn Alevander James De Nholm, ambaye anamtaka azuiwe kujihusisha na mali hiyo wakisubiri uamuzi wa mzozo wa umiliki wake.

Wawili hao walikutana mjini Thika na kuanza uhusiano kwa matarajio ya kuingia katika ndoa kihalali, lakini hilo halikutimia. Wakati wa uhusiano wao, Bw James anasema, alikuwa wazi kwa mwanamke huyo na alimhusisha katika mipango yake ya uwekezaji. Anasema, alinunua hata magari mawili na kumruhusu mwanamke huyo kuyatumia.

Karatasi za mahakama zinaonyesha kuwa, mnamo 2017, Bi Muema alimjulisha mgeni huyo mali iliyokuwa ikiuzwa eneo la Mtwapa, kaunti ya Kilifi. Walipotembelea eneo hilo, Bw De Nholm alivutiwa na kununua ardhi kwa Sh2.5 milioni.

Alinunua ardhi hiyo kumdhihirishia mwanamke huyo kuwa alijali uhusiano wao na alitarajia kuwa wangeoana. Kwa hivyo alijumuisha jina la mwanamke huyo katika makubaliano ya uuzaji. Baada ya kulipia ardhi hiyo, raia huyo wa kigeni alianza kujenga nyumba.

Baada ya muda, waliachana na mwanamke huyo kwa sababu ya kutoaminiana. Kisha alirudi Uingereza mnamo Juni mwaka jana.

Aliporudi Kenya baadaye, Bi Muema alimzuia kuingia katika nyumba hiyo na kufungia vitu vyake vya kibinafsi ndani ya nyumba.

Kitendo hiki kilimfanya kuandikia wakili aliyetengenza hati ya ununuzi wa hilo shamba, ambayo hakupewa. Alipouliza kwenye afisi za Usajili wa Ardhi, aligundua kuwa mali hiyo ilikuwa imesajiliwa kwa jina la mwanamke huyo. De Nholm analalamika kwamba mwanamke huyo pia alisajili magari yote kwa jina lake. “Vitendo vya mwanamke kusajili mali kwa jina lake ni kinyume cha sheria,” alimwambia Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Mombasa Francis Kyiambia, anayesikiliza kesi hiyo.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, De Nholm alisema aligundua kuwa mwanamke huyo alikuwa akimdanganya kwamba wangeoana, ili kumshawishi afanye uwekezaji naye baada ya mwanamke huyo kusajili mali zote kwa jina lake.

Kupitia wakili wake Collins Ondeng, mlalamishi huyo alisema alikuwa tayari kusajili mali hizo kwa pamoja kwa majina yao, lakini kwa kuzingatia mwenendo wake haramu, hayuko tayari tena kumsajili mwanamke huyo kama mmiliki wa pamoja wa mali hizo.

“Alishirikiana na wakili wake kufanya ulaghai na upotoshaji kwa nia ya kuninyima haki yangu ya umiliki wa mali hiyo,” alisema, akifafanua kwamba hakumnunulia Bi Mueni ardhi hiyo kama msamaha.

Mwanamke huyo kwa upande wake anakubali kwamba walikuwa katika uhusiano na jamaa huyo na walikusudia kuhalalisha ndoa.

“Lakini niligundua kwamba, De Nholm alikuwa ameoa kihalali na mwanamke mwingine Mkenya,” alielezea. Alionyesha vyeti vya ndoa ili kuthibitisha madai haya. Bi Muema alizidi kuarifu korti kuwa ni mgeni huyo aliyemshawishi ahamie Mtwapa, ambapo alidai angemtembelea wakati wowote akiwa nchini kwa likizo.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Desemba 17.

  • Tags

You can share this post!

Utata wazidi kuzingira kifo cha seneta wa Machakos

Kaunti 13 kuvamiwa na nzige tena – Katibu