Habari Mseto

Mhadhiri wa MKU atuzwa kwa ubunifu wake

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

MHADHIRI mmoja wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), ametambuliwa kama mbunifu wa kutegemewa kwenye kongamano moja lililofanyika nchini Rwanda hivi majuzi.

Bw Donatus Njoroge, aliteuliwa mshindi wa tuzo ya kimataifa iliyobuniwa na kitengo cha Kenya National Innovation Agency kwa mwito wa kufuatilia ajenda kuu nne za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Tuzo ya ubunifu huo inalenga kitita cha Sh800,000 ambazo zinawasilishwa kupitia MKU.

Ubunifu huo kwa jina ‘Molepse Bio-Resources and Novel Bio Pesticide’ ni mpango wa kuzuia wadudu waharibifu wa mimea na mavuno, ulishinda tuzo nyingine kupitia teknolojia mwaka wa 2017.

Mpango huo wa kiteknolojia umefadhiliwa na Shirika la United States Agency for Intenational Development (USAID).

Mbunifu mashuhuri

Bw Njoroge ambaye ni mhadhiri wa kutegemewa MKU, alitambuliwa kama mmoja wa wabunifu mashuhuri huku akikamata nafasi ya tano katika kongamano lililofanyika mwishoni mwa mwaka 2018 nchini Rwanda.

Kongamano hilo lilijumuisha wasomi wengi kutoka vyuo kadha kutoka maeneo tofauti ulimwenguni.

Baada ya kutambulika kama mmoja wa wanateknolojia mashuhuri ameorodheshwa katika semi-fainali kwa mashindano yajayo yatakayofanyika maeneo mengine ulimwenguni.

“Ili kufikia kiwango hicho inakujuzu kujinyima na kujitolea mhanga. Inahitaji pia kufanya utafiti wa kina na kujiamini. Na kwa yote, inahitaji kuweka Mungu mbele,” alisema Bw Njoroge.

Anasema yeye kama mhadhiri wa kutegemewa na MKU, atafanya juhudi kuona ya kwamba wanafunzi wote wanaopitia mikononi mwake wanapiga hatua zaidi kwa kuwa wabunifu na watu wa kutegemewa siku za usoni.

“Bara la Afrika halina upungufu wa ubunifu wa kuendeleza elimu lakini linahitaji watu wenye maono na waliojitolea kujituma kufanya utafiti na kujitokeza na mawazo mapya yanayoweza kuongeza mambo mengi ya kielimu,” alisema Bw Njoroge.