• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Mhariri wa KTN anayedaiwa kuiba Mercedez Benz asukumwa ndani

Mhariri wa KTN anayedaiwa kuiba Mercedez Benz asukumwa ndani

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mhariri wa habari katika Kituo cha Televisheni cha KTN  Bw Aaron Ochieng alisukumwa ndani Jumanne baada ya kushindwa kumlipa mtangazaji wa kituo hicho Bi Doreen Biira Sh1.2 milioni.

Bw Ochieng aliwekwa korokoroni na hakimu mkuu Bw Francis Andayi baada ya kushindwa kulipa pesa hizo kama walivyokuwa wamekubaliana na Bi Biira.

Mwanahabari huyo anakabiliwa na shtaka la wizi wa gari la Bi Biira aina ya Mercedez Benz. Kulingana na makubaliano yao , Bw Ochieng alikuwa amlipe mlalamishi huyo ndipo aondoe kesi dhidi yake. Alishtakiwa kuiba gari hilo lenye thamani ya Sh2.8 milioni miaka miwili iliyopita.

Kesi ilipotajwa Jumatatu ndipo Bw Ochieng aeleze ikiwa amekamilisha kulipa pesa hizo, korti iliambiwa hajakamilisha.

Hakimu aliamuru dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu alizokuwa amelipa kortini ndipo aachiliwe zitwaliwe na korti ndipo Bi Biira afike mahakamani kuzichukua.

Bw Andayi alielezwa kiwango cha Sh550,000 ndicho kimesalia kulipwa. Mshtakiwa alimsihi hakimu amruhusu akamalishe malipo lakini ombi lake likagonga mwamba.

“Sitakubali ombi lako upewe miezi mingine miwili ukamilishe malipo ya gari hilo,” Bw Andayi alisema.

Mhariri huyo alimwomba msamaha Bi Biira ili kesi dhidi yake iondolewe. Lakini Bi Biira aliweka masharti kuwa anataka alipwe ndipo aondoe kesi.

Bw Ochieng alikuwa amehahidi atakuwa analipa Sh350,000 kila mwezi.

Kwa kukosa kutimiza ahadi yake, mwanahabari huyo aliwekwa ndani hadi Juni 5, 2018 ambapo maagizo zaidi yatatolewa na mahakama.

You can share this post!

Kizimbani kwa kupanga kuilipua Mahakama Kuu ya Milimani

Nimeafikia lengo langu la kwanza Supa Ligi, asema Makumbi

adminleo