Miaka 30 jela kwa kuruhusu bangi ya mlanguzi ilale nyumbani kwake
MWANAUME mwenye umri wa miaka 45 amefungwa miaka 30 gerezani au alipe Sh50 milioni kwa kusaidia mlanguzi wa dawa ya kulevya kuficha magunia 63 ya bangi katika boma lake.
Benard Waguru Mwangi alipokezwa adhabu hiyo kali na Hakimu Mkaazi wa Nyandarua Lansatos Lorabi. Mwangi atatumikia adhabu hiyo kutokana na tamaa ya pesa kwa kuwa alilipwa Sh5,000 na mlanguzi aliyeficha bangi katika boma lake mnamo Januari 18, 2024.
Thamani ya bangi hiyo ni Sh41 milioni na kilichomchongea Mwangi zaidi ni kuwa alitoa ushahidi ambao unakinzana wakati ambapo kesi hiyo ilikuwa ikiendelea.
Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, polisi watano ambao walipata bangi hiyo na kumkamata walitoa ushahidi na Mwangi hakuwauliza maswali.
Polisi hao walisema kuwa walipata bangi ikiwa imefunikwa kwa mabati na mbao. Mwanzoni Mwangi alisema mwanaume alikuwa ameweka kontena kwake baada ya kumlipa Sh5,000
Alibadilisha kauli tena na kusema kuwa Sh5,000 ambazo alikuwa amelipwa na mtu huyo zilikuwa za kubadilisha umiliki wa shamba. Hata hivyo, alishindwa kutoa rekodi zozote za shamba ambalo lilikuwa linabadilishiwa umiliki.
Tena alibadilika na kusema kuwa alilipwa pesa hizo kutokana na kipande cha ardhi alichokuwa akiuza.
“Mtu ambaye anasaidia kufanikisha mwengine kutekeleza uhalifu ni sawa na mtu huyo na adhabu yake haifai kuwa tofauti,” akasema Hakimu Lorabi.
Kwa kuwa Mwangi alishindwa kuthibitisha ushahidi wake na hakupiga ripoti kwa polisi kuhusu kontena hiyo, ilikuwa wazi alikuwa akisaidia mlanguzi huyo wa bangi.
Kesi hiyo ilianza kusikizwa mnamo Julai 18. Karatasi ya mashtaka ilionyesha kuwa Mwangi, pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani walihusika na kuficha na kusafirisha gramu 1422,000 ya bangi.
Kontena hiyo yenye bangi ilipatikana nyumbani kwake eneo la Kigumo, Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.