Habari Mseto

Mifereji na mabwawa kujengwa Garissa kutatua tatizo la mafuriko

June 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

MIFEREJI na mabwawa yatajengwa katika Kaunti ya Garissa kama hatua ya kukabiliana na tatizo la mafuriko katika eneo hilo, Gavana wa Kaunti ameamua baada ya kukutana na Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji.

Akizungumza baada ya mkutano huo ulioandaliwa Jumatatu, Gavana Ali Korane alisema eneo hilo limeathiriwa vibaya na mafuriko tangu mwaka wa 1961.

“Wataalam wa kiufundi kutoka katika kaunti na serikali ya kitaifa watatoa rasilimali na kushirikiana na wengineo kutafuta suluhu la tatizo ya mafuriko,” alisema.

Gavana na timu ya WARMA, walisema mabwawa na mifereji ndiyo ufumbuzi na suluhisho muhimu la kupunguza athari za mafuriko ya mara kwa mara ambayo yamesababisha msukosuko katika eneo hilo.

“Kaunti imekuwa ikikumbwa na mafuriko mabaya zaidi na kusababisha upotezaji mkubwa kwa wakulima ambao wamekuwa kwenye kilimo cha mazao kando ya Mto Tana. Ni wakati wa kutafuta suluhisho,” gavana huyo alisema.

Akaongeza: “Zaidi ya jadi 100 na mazao yameathirika kutokana na mafuriko ya hivi majuzi. Ni dhahiri kuwa tunafaa kutafuta suluhisho la kudumu na linalofaa ili kumaliza athari hasi za mafuriko.”

Mei 2020 Mto Tana ulivunja kingo zake tena kama miaka ya awali na kuacha familia nyingi bila makao na kukaa kwenye kambi za watafuta hifadhi (IDP).