• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Miguna: Serikali yaitwa kortini Januari 21

Miguna: Serikali yaitwa kortini Januari 21

Na Richard Munguti

KIZUGUMKUTI kinakumba marejeo ya mwanaharakati Dkt Miguna Miguna baada ya mwanasheria mkuu Paul Kihara kutofika mahakamani Jumatatu kutoa mwangaza kuhusu masuala kadha ya kisheria.

Kutofika kortini Bw Kihara kulimwacha Dkt Miguna katika hali ya sintofahamu iwapo atawahi kurudi nchini.

Lakini Jaji John Mativo alimwamuru Bw Kihara afafanue kuhusu masuala yaliyokanganya kuhusu maagizo ya kumtaka afike kortini.

“Kile hii mahakama ilitaka ni Bw Kihara kufafanua iwapo maafisa wanaohusika watafanikisha kurudi kwa Dkt Miguna au la,” alisema Jaji Mativo.

Jaji huyo alieleza katika uamuzi wa jana kwamba mwanasheria mkuu ndiye mshauri mkuu wa maafisa wa serikali katika masuala yote ya kisheria.

Pia alisema mwanasheria mkuu ni rafiki wa mahakama na anatakiwa kutoa mwelekeo kuhusu masuala nyeti ama yale yanayokanganya ya kisheria.

“Mwanasheria mkuu kama mshauri wa Serikali yuko na ufahamu mpana wa masuala ya kisheria kwa hivyo kufika kwake kortini kutatoa mwanga anayepasa kutekeleza maagizo ya korti,” alisema Jaji Mativo.

Hivyo basi alimtaka mwanasheria mkuu afike kortini mwenyewe ama amtume mwakilishi wake Januari 21 2020 kueleza kilicho kigumu katika kutekeleza agizo la korti.

Mahakama ilisema iwapo maagizo ya mahakama yatakiukwa jinsi inavyoendelea basi hali na suitafahamu itakumba nchi hii.

Bw Kihara hakufika kortini jana kama alivyoagizwa Ijumaa bali alimtuma wakili wa Serikali Bw Emmanuel Mbita kufafanua kile mwanasheria huyu mkuu alitakiwa kufanya.

Jaji Mativo alifafanua kwamba , Bw Kihara au mwakilishi wake wanatakiwa kueleza sababu ya maafisa wakuu wa Serikali kukaidi agizo wafanikishe kurudi kwa Dkt Miguna.

Dkt Miguna yuko mjini Berlin Ujerumani anakosubiri Serikali itekeleze agizo la mahakama kuu ifanikishe kurudi kwake.

“Wakenya wenzangu mnaouliza hali yangu, nataka kuwaarifu mimi niko mzima kama kigongo. Niko mjini Berlin, Ujerumani nikisubiri maafisa wakuu serikalini watii agizo la mahakama kufanikisha kurejea kwangu Kenya,” Dkt Miguna alisema katika ujumbe aliotuma kwa mtandao wa Twitter.

Kufuatia agizo la Mahakama Dkt Miguna afanikishiwe kurudi msemaji wa Serikali , Kanali (mstaafu) Cyrus Oguna alimtaka mwanaharakati huyo awasiliane na mabalozi ya Kenya ng’ambo kupewa pasipoti nyingine.

Jaji Mativo aliamuru kesi hiyo itajwe Januari 13 2020 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Wanachuo wakabiliana na polisi wakipinga faini

Trump aonya Iran dhidi ya kuua waandamanaji

adminleo