Miili minne ya waliotoweka yapatikana mbugani Tsavo
MISHI GONGO na COLLINS OMULO
MIILI minne ya wanaume wanaodaiwa kutoweka mwaka 2019 katika hali ya kutatanisha Kaunti ya Kwale ilipatikana ikiwa imetupwa katika msitu wa Tsavo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa wanaume hao ni miongoni mwa waliotoweka baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama.
Kulingana na mashirika ya Haki Africa na Human Development Agenda (HUDA) wanaume hao walitoweka kati ya mwezi wa Novemba na Desemba mwaka 2019 baada ya kuchukuliwa na watu wanaodaiwa kuwa mafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini, ATPU.
Shirika la Haki Afrika lilisema mili hiyo ilitambuliwa kama ya Juma Said Sarai, Khalfan Linuku, Abdalla Nassir Gatana (Desemba 22) na Usama Nassir (Novemba 30).
Mkurugenzi wa Haki Afrika Hussein Khalid alisema miili hiyo ilipatikana kati ya Januari 19 na 20.
Bw Khalid alisema miili hiyo inayohifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Makindu, ilipatikana ikiwa na majeraha yalioonyesha kuwa wanne hao waliteswa kabla ya kuuawa.
“Miili hiyo ilikuwa na ishara ya kuteswa, ina vidonda vya moto na alama za kunyongwa. Baadhi yao walikuwa na kamba na mifuko ya nailoni iliyofungwa mikononi, miguuni na shingoni mwao,” alisema Bw Khalid.
Bw Khalid alisema familia za marehemu zilithibitisha ilikuwa ya jamaa zao.
Alisema kati ya mwaka 2018 na 2019 zaidi ya watu 56 katika eneo la Pwani wamepotea baada ya kutekwa na watu wanadaiwa kuwa maafisa wa kupambana na ugaidi.
“Iwapo mtu anashukiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi, tunaomba sheria ifuatwe. Watu hawa wanapaswa kupelekwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka na iwapo watapatikana na makosa, basi waadhibiwe kulingana na sheria,” akaeleza.
Alisema maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kaunti ya Kwale, Lamu na Mombasa.
Alisema bado wanaendelea kutambua miili katika mochari hiyo.
“Tunaendelea na shughuli ya kuangalia miili iliyookotwa mbuga ya Tsavo, tuna imani familia zaidi zilizopoteza wapendwa wao zitafanikiwa kupata miili yao,” akasema.
Alitoa mwito kwa serikali kuunda jopo litakalochunguza visa hivyo na kupatia haki familia za walioathirika.