Milly Glass ya Mombasa sasa kuhamia Ethiopia, watu 2,000 kupoteza ajira
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya kutengeneza vioo ya Milly Glass iliyo na makao yake Mombasa imepanga kuhamia Ethiopia.
Kutokana na mpango huo, huenda wafanyikazi 2000 wakapoteza kazi humo.
Kulingana na wamiliki wa kampuni hiyo, masoko ya Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Madola yameruhusu uagizaji wa bidhaa za bei ya chini kutoka kwa mataifa washirika.
Kampuni hiyo ilisema hali itakuwa mbaya zaidi ikiwa Kenya itatia sahihi mkataba mwingine kati yake na Afrika Kusini.
Mshauri wa kampuni hiyo Jumamosi alisema bidhaa za bei ya chini kutoka nje zimefanya biashara kuwa ngumu kwa kampuni za humu nchini.
Kampuni hiyo imekuwa ikihudumu humu nchini kwa miaka 40 sasa na ilikuwa imepanga kupanua operesheni zake kufikia Julai 2019 kwa gharama ya Sh600 milioni.
Ikiwa utafiti utaonyesha kuwa hali haitaimarika, kampuni hiyo itavunjilia mbali mpango huo.
Kampuni hiyo imeanza ujenzi wa kiwanda kwa gharama ya Sh48 milioni Ethiopia.