Habari Mseto

Mipango ya mazishi ya Murunga bado yaendelea

November 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

SHABAN MAKOKHA na RICHARD MUNGUTI

MIPANGO ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Matungu, Justus Murunga inaendelea katika kwake jijini Nairobi na Mumias licha ya agizo la mahakama la kusitisha mazishi.

Jumamosi, kamati ya bunge inayoshughulikia mazishi hayo ilisema mazishi hayo yamepangwa kufanyika Novemba 28, 2020.

Wanachama wa kamati hiyo, Cleophas Malala, Benjamin Washiali na Bernard Shinali walitembelea kaya za marehemu katika kijiji cha Makunda eneo la Matungu na Makutano eneo la Lugari na kukutana na watu wa familia kupanga mazishi.

“Tumekubaliana na familia kwamba mambo yakienda sawa, tutamzika ndugu yetu Novemba 28. Maspika wa mabunge yote mawili wamekubaliana nasi,” alisema Bw Washiali.

Alisema mawakili wa bunge watakata rufaa uamuzi wa kusimamisha mazishi na wakikosa kufaulu, wataahirisha siku ya mazishi.

Wakati huo huo, wajane wawili wa Murunga sasa wanataka mwanamke aliyewasilisha kesi ya kusimamisha mazishi aweke dhamana ya Sh10 milioni kortini zitakazogharimia kesi na mazishi.

Bi Christabel Jane na Grace Murunga wanasema iwapo hataweka dhamana hiyo, mahakama iwaruhusu wakazike mwili wa mume wao Novemba 28, 2020.

Katika kesi waliyowasilisha Ijumaa alasiri, wajane hao wanaomba korti ifutilie mbali agizo la kusitisha mazishi hayo wakisema itakuwa ni gharama kubwa mazishi hayo kutofanyika ilivyopangwa.

Mahakama iliamuru mochari ya Lee Funeral isiachilie mwili wa Murunga hadi kesi iliyowasilishwa na Agnes Wangui Wambiri anayedai kuwa mke wa tatu wa marehemu isikizwe na kuamuliwa.

Christabel na Grace wamesema hawamjui Agnes Wangui Wambiri wala watoto wake wawili.