Mishra pabaya kwa kuunga Duale atoke
Na ONYANGO K’ONYANGO
MBUNGE wa Kesses, Dkt Swarup Mishra amejipata matatani baada ya wafuasi wa Naibu Rais, Dkt William Ruto katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kumtaja kama msaliti kwa kutia saini hoja iliyomwondoa aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Bw Aden Duale.
Wakazi hao walieleza Taifa Leo kwamba walishangazwa na hatua ya mbunge huyo kutia saini hoja ya kumtimua Bw Duale katika nafasi yake.
Aidha, walisema hawataendelea kuvumilia siasa za mbunge huyo huku wakiahidi kutompigia kura tena katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.
Bw Daniel Kering aliwaongoza wakazi hao kwa kumrejelea Dkt Mishra kama msaliti, akisisitiza eneo hilo ni ngome ya Dkt Ruto na hakuna kiongozi yeyote anayefaa kuenda kinyume na maagizo yake.
“Mbunge wetu ametusaliti baada ya kubainika kwamba alikuwa kati ya wabunge waliotia saini hoja ya kumbandua Bw Duale ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto. Hatutampigia kura tena kama mbunge wetu 2022,” akasema.
Kwa mujibu wa Dkt Mishra, alikuwa kati ya wabunge waliotia saini hoja hiyo kwa sababu hakutaka kuenda kinyume na maagizo ya chama alichotumia kuwania ubunge mnamo 2017.
“Ndiyo nilitia saini hoja ya kumbandua Duale kwa sababu chama kilitaka atimuliwe,” akasema Bw Mishra katika eneobunge lake mnamo Jumapili.
Vilevile wakazi hao sasa wanadai kwamba mbunge huyo alisaini hoja hiyo ili kumridhisha Rais Uhuru Kenyatta ndipo asitimuliwe kama Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Afya bungeni.
Walisema anatumia uanachama wake kwenye kamati hiyo ili kuendesha shughuli katika hospitali zake za Mediheal zinazopatikana kote nchini.
“Dkt Mishra amedhihirisha siasa za uvuguvugu dhidi ya Naibu Rais kwa muda mrefu. Hata hivyo, Jumapili aliweka mtazamo wake hadharani na kusema alishiriki juhudi za kumng’oa Duale ili asalie kwenye wadhifa wake wa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo. Alifanya hivyo ili Rais asimtimue kwenye wadhifa huo anaotumia kuendesha hospitali zake,” akasema Bw Domnic Kibet kutoka Kesses.
Katika ngome ya Naibu Rais ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa, sasa ni wazi kwamba Dkt Mishra na Naibu Spika, Prof Margaret Kamar ambaye pia ni Seneta wa Uasin Gishu, ndio wandani wa Rais Kenyatta.
Kinaya ni kwamba Dkt Mishra, kabla ya kubanduliwa kwa Bw Duale, alikanusha vikali kwamba alikuwa kati ya wanasiasa walioshirikiana na mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega kusaini hoja dhidi ya Bw Duale.
Mwanasiasa huyo alisema hiyo ilikuwa njama ya wapinzani wake kugharimia sifa.
Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany naye alisema uteuzi wa Bi Kamar kama Spika ni pigo kuu kwa demokrasia nchini huku baadhi ya wenyeji wakimrejelea kama msaliti.
“Hatutaendelea nchini iwapo watu watatumika na kushawishiwa kutwaa nyadhifa ambazo washikilizi wao walivuliwa mamlaka kwa njia isiyofaa,” akasema Bw Kositany.
Hii si mara ya kwanza Dkt Mishra anajipata matatani.
Hivi majuzi alitofautiana na maafisa wa usalama kuhusu namna alivyokuwa akisambaza chakula cha msaada eneobunge lake bila kufuata kanuni za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.