Habari Mseto

Mitihani ya majaribio yaanza

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WANAFUNZI wa Gredi ya Nne na wenzao wa Darasa la Nane, Jumatano wameanza mitihani ya majaribio iliyoandaliwa na Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC).

Kulingana na kaimu afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo, Mercy Karogo, mitihani hiyo inalenga kutathmini ikiwa wanafunzi hawa wangali wanafahamu yale waliyofundishwa kabla ya shule kufungwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 nchini mnamo Machi 15, 2020.

“Mitihani hiyo ya majaribio pia inakusudiwa kuwafanya wanafunzi warejeshe mawazo yao katika mazingira ya masomo ya kawaida baada ya wao kukaa nyumbani kwa kipindi cha miezi saba. Kila mwanafunzi anatathminiwa kubaini kiwango chake cha kung’amua masomo yaliyoko kwenye mtaala,” akaeleza Bi Karogo.

Mitihani hiyo itaendelea hadi Jumatatu, Oktoba 26. Katika siku ya kwanza wanafunzi wa Darasa la Nane walianza kwa kufanya mtihani wa Hisabati, Lugha ya Kiingereza na Insha ya Kiingereza.

Mitihani ya masomo ya Sayansi, Lugha ya Kiswahili na Insha ya Kiswahili itafanywa siku ya pili huku Somo la Kijamii likitahiniwa siku ya tatu, ambayo ni Jumatatu, Oktoba 26, 2020.

Mitihani ya Gredi ya Nne itaendeshwa kwa siku nne ambapo Somo la Kiingereza, kuongea na kusoma, itafanywa siku ya kwanza.

Katika siku ya pili, wanafunzi watatathminiwa katika Kiingereza, kusoma, kukumbuka na kuandika.

Nyanja zingine ambazo wanafunzi wa Gredi ya Nne watatathminiwa ni mazingira, sayansi na teknolojia.

Katika siku ya tatu, wanafunzi watathminiwa katika Somo la Kiswahili, vitengo vya kusikiza, kuongea na kusoma kwa sauti. Mtihani wa sarufi ya Kiswahili na uandishi wa matini ya lugha hii utafanyika siku ya nne.

Wizara ya Elimu haijatangaza tarehe ambapo wanafunzi wa madarasa mengine watarejelea masomo wakati huu ambapo visa vya maambukizi ya virusi vya corona vinaongezeka.

Waziri wa Elimu George Magoha alisema hatua hiyo, ya kuwaita wanafunzi wengine, itategea hali ya maambukizi ya Covid-19 humu nchini.