• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Mjane aliyefurushwa kufuatia mzozo na wake wenza arejea kwa nyumba yake

Mjane aliyefurushwa kufuatia mzozo na wake wenza arejea kwa nyumba yake

NA SAMMY KIMATU

MAMA mmoja mjane ambaye amekuwa akihangaika kwa miezi minane katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo kwa kufungiwa nje na kufukuzwa kutoka kwa nyumba yake na wenzake wawili katika mtaa wa Golden Gate, hatimaye amerudi nyumbani kwake.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya kipekee, Naibu Kamishna wa Starehe John Kisang alisema Bi Winickister Wandela Waithera,43, alipitia machungu baada ya kufukuzwa na wake wenza wawili baada ya mumewe, Bw Peter Amollo Akumu Gould kuaga dunia.

Bw Kisang alisema mama huyo alikuwa amefungiwa kufuli na maafisa wa utawala baada ya kesi ya mzozo wa nyumba baina yake na wajane hao wengine kuamuliwa kimakosa na machifu wa awali waliostaafu.

Aliongeza kwamba wanawake hao waling’ang’ia mali ya marehemu mume wao.

Mali hiyo inakisiwa kuwa ya thamani ya zaidi ya Sh200 milioni.

Bw Kisang alieleza kwamba baada ya maagizo ya korti kwa maafisa wa utawala kwamba Bi Waithera alikuwa ameunganishwa na wenzake wawili kupitia kuwa wake wa mume huyo mmoja kabla ya kifo chake, hivyo ana haki ya kupewa nafasi katika umiliki wa mali ya marehemu.

Bw Kisang aliangiza msaidizi wa kamishna katika tarafa ya South B, Bw Solomon Muranguri kutekeleza agizo la mahakama kwamba Bi Waithera lazima afurahie mali ya marehemu sawa na wenzake wanaposubiri uamuzi wa korti kuhusu jinsi watakavyogawana mali ya marehemu.

“Bi Waithera alienda kortini na kulalamika kutupwa nje kutoka kwa nyumba yake katika mtaa wa Golden Gate-South B. Korti imenipa kibali cha kuhakikisha mlalamishi anarudi kwa nyumba yake kwani yeye ni mjane sawa na wenzake wawili hivyo wote watatu wanasubiri uamuzi wa korti jinsi mali ya marehemu mume wao itakavyogawanywa,” Bw Kisang akasema.

Alisema machifu waliokuwepo miaka ya awali walikosea katika kutoa uamuzi wa kuweka kufuli nyumba ya Bi Waithera ndiposa uamuzi huo umebatilishwa.

Kulingana na stakabadhi zilizoonekana na Taifa Leo, Bi Waithera ni mke wa tatu wa marehemu. Mke wa pili anajulikana Bi Celina Awino Awuor japo mke wa kwanza hajatajwa jina.

“Watoto wa mke wa pili waliungana na mke wa kwanza kumfukuza Bi Waithera kutoka mtaa wa Golden Gate na wakachukua watoto wawili wa Bi Waithera ili wabaki katika nyumba hiyo,” Bw Muranguri alisema.

Wakati wa kuangazia kwa kina kuhusu mzozo huo, Bw Muranguri alifichua kwamba chifu aliyehusika kutatua mzozo huo alichukua fundi wa kuchomelea vyuma na ndipo wakamfungia mlalamishi nyumba yake kwa kufuli na kisha kuchomelea mlango wa chuma kumnyima mwanya wa kuingia ndani ya nyumba yake.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wachunguza vifo vya watu wawili Makadara

Polisi wasaka mwanamume aliyetoa orodha ya anaolenga kuua

T L