• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mkahawa wapiga marufuku sahani, chupa na vijiko vya plastiki

Mkahawa wapiga marufuku sahani, chupa na vijiko vya plastiki

Na Eunice Murathe

MKAHAWA umepiga marufuku matumizi ya chupa, vijiko na sahani za plastiki kama njia mojawapo ya kulinda mazingira.

Hoteli ya MNkafe iliyoko jijini Mombasa ilitangaza kuwa kuanzia kesho haitawahudumia wateja wake chakula kwa kutumia sahani, vijiko na chupa za plastiki.

“Kuanzia Agosti 15, 2018, hoteli ya MNKafe haitawahudumia wateja kwa kutumia vifaa vya plastiki. Japo kutakuwa na changamoto mwanzoni katika utekelezaji wa uamuzi huo, tunaamini kuwa sote tutanufaika katika siku za usoni,” ikasema taarifa ya hoteli hiyo.

Ilisema sasa itatumia sahani, vijiko, vikombe ambavyo havidhuru mazingira badala ya plastiki.

Mkurugenzi wa hoteli hiyo Muhammad Nazir alisema walichukua hatua hiyo baada ya kutazama video katika mitandao ya kijamii iliyoonyesha madhara ya matumizi ya vifaa vya plastiki vinapoingia ziwani au baharini.

“Badala ya kutumia plastiki sasa tutatumia vifaa vilivyotengenezwa kwa miti. Tutahudumia maji wateja kwa chupa za glasi,” akasema.

Mkahawa huo pia ulisema kuwa utapiga marufuku ya matumizi ya mirija ya plastiki kunywa soda.

“Tutapiga marufuku matumizi ya mirija kuanzia mwezi ujao, tutatumia mirija mbadala iliyotengenezwa kwa miti,” akasema.

“Tumeona madhara ambayo vifaa vya plastiki vinasababisha baharini. Mkahawa wetu ni mdogo na tunatarajia kuwa hata mahoteli ya kifahari yataiga mfano wetu ili tuboreshe mazingira kwa pamoja, “ akasema Bw Nazir.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Pwani Najya Muhammed, alipongeza hatua ya mkahawa huo alisema vifaa vya plastiki, haswa vinapotumiwa mara moja na kutupwa, baadaye huishia baharini na kudhuru samaki na viumbe vinginevyo vilivyoko majini.

  • Tags

You can share this post!

Purukushani walimu wakuu wakimrushia chupa Ndolo kupinga ada

Maraga amkaribisha kinara mpya wa PSC kusaidia kutatua kesi...

adminleo