Mkandarasi wa ujenzi barabara ya Lamu-Garsen asitisha shughuli kwa kuhofia kushambuliwa na al-Shabaab
Na KALUME KAZUNGU
MKANDARASI wa ujenzi wa barabara ya Lamu kuelekea Garsen amesitisha shughuli zake kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi wake kufuatia shambulio la Jumapili ambapo wapiganaji wa al-Shabaab walichoma magari mawili eneo hilo.
Barabara ya Lamu-Garsen inajengwa na kampuni ya H-Young.
Mradi huo uliokadiriwa kugharimu serikali Sh10.8 bilioni ulianzishwa tangu Machi 2017 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2020.
Baadhi ya vibarua wa kampuni ya ujenzi ya H-Young waliohojiwa na ‘Taifa Leo’ walikiri kutumwa nyumbani na usimamizi wa H-Young hadi pale watakapohakikishiwa usalama wao.
“Tuliamriwa kwenda nyumbani tangu Jumapili muda mfupi baada ya tingatinga la H-Young na lori la kubeba saruji kuteketezwa na al-Shabaab eneo la Milihoi,” akasema mmoja wa vibarua hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alithibitisha Alhamisi kusitishwa kwa shughuli za ujenzi wa barabara hiyo lakini akasema ofisi yake tayari inafanya mazungumzo na usimamizi wa H-Young ili kuona kwamba shughuli za ujenzi wa barabara hiyo zinarejelewa kama kawaida.
“Wafanyakazi wa H-Young wamesitisha ujenzi wa barabara ya Lamu-Garsen kwa sababu za kiusalama. Tuko mbioni kuzungumza na usimamizi wa H-Young ili kurejelea shughuli zao kwani usalama umedhibitiwa vilivyo Lamu na hakuna la kuhofia kwa sasa,” akasema Bw Macharia.
Kamishna huyo aidha aliwasisitizia wakazi kuwa macho na kupiga ripoti kwa walinda usalama endapo watashuhudia tukio au mtu yeyote wanayemshuku kuwa kero kwa usalama wa nchi.
Mnamo Januari 7, 2020, zaidi ya vibarua 2,000 wanaoendeleza ujenzi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) walitumwa nyumbani kufuatia hofu ya mashambulio ya al-Shabaab.
Hii ni baada ya wapiganaji hao kutekeleza uvamizi wa kambi ya jeshi ya Manda-Magogoni ambayo ni takriban kilomita moja kutoka eneo la Kililana ambako mradi wa LAPSSET unaendelezwa.
Wafanyakazi hao hata hivyo walirudishwa kazini wiki chache zilizopita.