• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Mkenya aliye Canada asimulia hali ilivyo

Mkenya aliye Canada asimulia hali ilivyo

Na GEOFFREY ANENE

Fanice Mokeira ni mhudumu wa afya nchini Canada. Nchi hiyo imeshuhudia visa 16,667 vya maambukizi ya virusi vya corona. Watu 323 pia wamepoteza maisha nchini humo kutokana na ugonjwa wa Covid-10 unaosababishwa na virusi hatari vya corona.

Taifa Leo l]ilipata kuzungumza na Mokeira kufahamu anavyokabiliana na maisha wakati huu mgumu, ambao visa 1, 363, 123 vya maambukizi ya virusi hivyo na vifo 76, 383 vimethibitishwa kote duniani.

Nimeishi Canada miaka 10. Mimi ni mkazi wa mji wa Ontario. Nchini Canada, tunazungumza Kiingereza na Kifaransa. Taaluma yangu ni mhudumu wa afya kwa hivyo mimi niko mstari wa mbele na katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi hivyo. Nahudumia watu wazee na wale walio na ulemavu katika jamii. Sheria inasema sisi wahudumu wa afya hatuwezi kukaa nyumbani wakati kama huu ambao tunahitajika zaidi. Hata hivyo, uamuzi wa kuenda kazini ama la ni wa mtu binafsi.

Njia moja ambayo nimeathirika na janga hili ni kuwa nina watoto watatu, ambao hubaki nyumbani kwa sababu shule zimefungwa. Kwa sababu ya hofu ya maambukizi pamoja na magumu ni menginine mengi, hawawezi kuenda nje ya nyumba.

Bei ya bidhaa haijaongezeka hapa na ikiwa imepanda, basi ni kwa kiasi kidogo sana.

Wakati siko kazini, mimi napenda kutumia muda wangu wote na watoto wangu. Lazima niwaweke katika hali ya utimamu wa akili wakati huu mgumu. Watoto wangu wanapenda sana kutumia mitandao ya kijamii.

Shule pia zinawapatia masomo kupitia mitandao kwa hivyo wakati mwingine mimi nasoma nao, ingawa ni kazi ngumu na ambayo inaweza kuwa isiyopendekeza. Serikali imesaidia wazazi kwa kuwapatia vipakatalishi na intaneti kufanisha masomo nyumbani.

Virusi vya corona ni hatari. Kama si lazima uende nje ya nyumba, tafadhali usiende. Kaa nyumbani. Nunua vyakula vinavyopatikana kwa bei rahisi kama mchele na maharagwe. Kula vyakula hivi sana. Jiweke salama kwa sababu dunia nzima inaumia sio tu Wakenya.

You can share this post!

SHAIRI: Corona janga hatari, limetunyima raha

CORONA: Mwanahabari aliyetamani kuzuru Kenya

adminleo