Mkewe Mwangi Wa Iria ajipata pabaya kwa ufisadi wa Sh351m
NA RICHARD MUNGUTI
MKEWE aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, Jane Waigwe Kimani ameshtakiwa kwa kula njama za kuilaghai kaunti hiyo zaidi ya Sh351 milioni.
Jane alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Victor Wakhumile katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani.
Mkewe huyo gavana wa kwanza kaunti ya Murang’a, alishtakiwa pamoja na Bw David Maina Kiama kwa kula njama hizo za kuilaghai kaunti mamilioni hayo kati ya Oktoba 21, 2014, na Juni 19, 2017.
Katika stakabadhi ya mashtaka, Jane ameshtakiwa pamoja na mumewe wa Iria, Patrick Kagumo Mukuria, Jane Wanjiru Mbuthia, David Maina Njeri, Solomon Mutura Kimani na Peter Muturi Karanja.
Hakimu alifahamishwa kwamba Mukuria alikuwa Katibu wa Kaunti ya Murang’a na Karanja alikuwa msaidizi wa gavana.
Washtakiwa hao wengine walikuwa wakurugenzi wa Top Image Media Consultants na Value View Limited.
Jane na Kiama walikanusha mashtaka dhidi yao kisha wakaomba kuachiliwa kwa dhamana.
Mawakili Wilfred Nyamu na Peter Wanyama walieleza mahakama kwamba kesi dhidi ya washtakiwa hao ni sawa na ile iliyoshtakiwa wa Iria Aprili 30, 2024, na akaachiliwa kwa dhamana.
“Naomba hii mahakama iwaachilie washtakiwa kwa dhamana. Watafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi. Hawatatoroka,” Bw Nyamu alimweleza Wakhumile.
Jane alikabiliwa na mashtaka saba ya kula njama za kuifuja kaunti ya Murang’a Sh351,097,491.
Shtaka lilisema pesa zilikuwa malipo ya huduma zilizotolewa kwa kaunti hiyo na kampuni ya Top Image Media na View Value Limited.
Jane alikabiliwa na mashtaka mengine manne ya ubadhirifu wa pesa.
Jane na kampuni za Top Image Media Consultants Limited na Value View Limited walishtakiwa kujipatia Sh7.5 milioni walizotumia kununua jumba katika mtaa wa Umoja Innercore.
Mahakama ilielezwa pesa hizo zililipwa kimakosa kutoka kwa akaunti za gatuzi la Murang’a.
pia mke huyo wa gavana alikana shtaka lingine la kupokea Sh4.4 milioni alizonunua nyumba mbili Batian 4 na Nellion 88 kupitia kwa akaunti ya Mlima Kenya Homes Account.
Jane alidaiwa alipokea kimakosa Sh3.7 milioni kutoka kwa kaunti hiyo na kuzitumia kununua shamba la ekari 13 katika eneo la Mweiga, Nyeri.
Pamoja na hayo Jane pia alikana alipokea Sh600,000 kutoka kwa gatuzi hilo kuchimba visima katika shamba hilo la Mweiga.
Bi wa Iria alishtakiwa kwa kupokea tena Sh3 milioni kwa niaba ya Top Image Media Consultants Limited mnamo Julai 1, 2014, zilizotoka kwa akaunti ya gatuzi la Murang’a.
Shtaka jingine lilisema kuwa Jane alipokea Sh500,000 kutoka kwa Top Image Media Consultants Limited akijua kampuni hiyo ilipokea kwa njia ya ufisadi pesa hizo kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Murang’a.
Akitoa uamuzi kuhusu ombi la dhamana, Bw Wakhumile aliamuru Jane na Kiama walipe dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja.
Kesi hiyo dhidi ya Jane itatajwa baada ya wiki mbili pamoja na ile inayomkabili mumewe wa Iria kwa maagizo zaidi.
Wa Iria alishtakiwa mnamo Aprili 30, 2024, na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh20 milioni ama alipe dhamana ya pesa taslimu Sh10 milioni.
Kinara mwenza wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, Kalonzo Musyoka, ndiye alimwakilisha wa Iria pamoja na Nyamu na wakili Njiru Ndegwa.
Bw Musyoka alimweleza Nzioki kwamba kesi hiyo aliyoshtakiwa Wa Iria ni ya kisiasa kwa vile imewasilishwa kortini miaka 10 baada ya mshtakiwa kuhudumu.
Wa Iria ndiye kinara wa chama cha kisiasa cha Usawa Political Party (UPP).