Habari Mseto

MKU yaandaa hafla ya kufuzu mahafali kupitia jukwaa la mtandaoni

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kiliendesha hafla ya kuhitimu kwa mahafali wake kupitia jukwaa la mtandaoni.

Mnamo Ijumaa zaidi ya wahitimu wapatao 4,000 walifuatilia hafla hiyo mtandaoni wakiwa sehemu tofauti.

Mwenyekiti na mwanzilishi wa chuo hicho Prof Simon Gicharu aliyesoma hotuba yake kupitia mtandaoni alipongeza wahitimu wote waliokuwa katika orodha hiyo ya waliofuzu huku alitoa shukrani zake za dhati kwa wahadhiri wote waliofanikisha mpango huo wote hasa wakati huu mgumu wa janga la Covid-19.

“Ninajua safari hiyo haikuwa rahisi hivyo, kwani wanafunzi wengi walitawanyika kote nchini na nchi za nje huku wakiwasiliana na wahadhiri wao kupitia mtandaoni. Natoa shukrani pia kwa wazazi kwa uvumilivu wao wakati huu mgumu wa corona,” alisema Prof Gicharu.

Alisema MKU imeonyesha wazi kuwa inafuata maagizo yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya na ndiyo maana ilipewa nafasi na serikali kuendesha mipango yake ya kufuzu kwa mahafali hao.

Alisema hafla hiyo ilifanikiwa kabisa kwa sababu wanafunzi na wazazi walifuatilia kupitia runinga ya TV 47 na stesheni zile zingine ambazo hupeperusha habari zao.

Alisema homa ya corona imefunza watu mengi ambapo kutoka wakati huu kuendelea mbele wanafunzi wengi watazingatia masomo kupitia mtandao kwa sababu huo ndio mtindo ambao utakumbatiwa zaidi ulimwenguni kote.

Alisema wakati huu wa Covid-19 wahadhiri kadha na wanasayansi wachache waliweza kubuni vifaa na mitambo mingi ambapo MKU ilijitokeza na kifaa cha kuwasaidia wagonjwa wa Covid-19 kupumua;  ventilator. Huo ulikuwa mchango mkubwa kwa chuo hicho.

Alipongeza juhudi za chuo hicho kufungua kitengo kingine cha masomo katika jiji la Kigali nchini Rwanda ambapo kwa wakati huu kimepata wanafunzi tayari.

Aliwashauri wananchi wasiogope homa ya Covid-19 lakini wajizoeshe kuielewa na kukabiliana nayo.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – ICT – Joe Mucheru aliyesoma hotuba yake kupitia mtandao aliwapongeza wahadhiri wote kwa kuwatayarisha wahitimu hao wote na kuweza kuafikia malengo yao.

“Ninaelewa wakati huu wa mlipuko wa homa ya corona kulikuwa na pandashuka nyingi lakini kwa sababu ya bidii na kujiamini wahitimu hao waliafikia malengo yao,” alisema Bw Mucheru.

Alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika maswala ya teknolojia ya ICT ambapo katika mwezi wa Januari 2020 kulikuwa na watumiaji wa mtandao zaidi ya 22 milioni.

“Teknolojia ya ICT imetufunza mengi na bila shaka ndiyo njia ya kipekee ya kuendeleza mambo yetu ya kisasa,” alisema waziri huyo.

Aliwahimiza watu popote walipo kuzingatia masomo kwa sababu “hiyo elimu ndiyo itatuondoa kutoka kwa ufukara.”

Chansela wa chuo hicho Prof John Struther ambaye pia alisoma hotuba yake kupitia mtandaoni, alipongeza wazazi, wahitimu na washika dau wote kwa kukubali kufuata mwongozo uliotolewa wa mtandao.

“Ninaelewa wengi wenu mlitamani kuwa pamoja na wana wenu katika hafla hiyo lakini kwa sababu ya shida iliyotukumba kote ulimwenguni tutalazimika kuvumilia yote,” alisema Prof Struther.

Alisema chuo hicho kimejizatiti na kupiga hatua kubwa kimasomo ikilinganishwa na vyuo vingine.

Aliwatakia wahitimu wote heri njema katika uwanja mkubwa wa kutafuta ajira akisema huu ndio wakati wa kujitambulisha kuwa tofauti na watu wengine kwa kuonyesha ubunifu kwa kufanikisha malengo yote yalio mbele yao.