Habari Mseto

Mmoja wa wasichana watatu waliotekwa nyara Garissa ajinasua

June 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

WASICHANA watatu walitekwa nyara Jumanne katika Kaunti ya Garissa karibu na maeneo yao ya nyumbani.

Wasichana hao wanasemekana wana umri wa kati ya miaka saba, 14 na 12.

Walakini, mmoja wa wasichana, mwenye umri wa miaka 12 alifanikiwa kujinusuru.

Akithibitisha tukio hilo baba ya msichana huyo, Abdullahi Mohammed alisema tukio hilo lilitokea karibu na eneo la Bula Iftin.

“Muda wa saa nne asubuhi mama yake alikuwa amemtuma kwa nyumba ya jirani kupeleka chupa ya maji lita tatu kwenye friji kwani hatuna moja. Lakini hakurudi na tukadhani yuko nje akicheza na marafiki zake,” alisema Bw Mohammed.

Anasema baada ya muda wa saa chache, walimtuma kakake mdogo kwenda kumtafuta.

“Msichana alikuwa hayuko kwa jirani na hapo ndipo mama yake alianza kumtafuta lakini naye akarudi bila mafanikio ya kumpata msichana huyo,” akasema Bw Mohammed.

Kulingana na taarifa ya msichana huyo, alitekwa mbele ya nyumba yao na wanaume wawili na mwanamke.

Alikamatwa, akapelekwa kwa gari na kunyunyuziwa kemikali kwenye uso.

“Alitufafanulia hakujua yote hadi kufikia daraja ambalo liko kati ya Madogo na Mororo ambapo kuna ukaguzi wa polisi. Wateka nyara wasiojulikana walikuwa wakizungumza na polisi wakati alifanikiwa kufungua mlango wa gari na kutoroka, akiwaacha wasichana wengine wawili wakiwa wamefungwa kwa kamba,” alisema baba huyo, kwani msichana huyo hakuruhusiwa kuongea na Taifa Leo.

Chifu wa eneo la Bula Iftin, Bw Deqow Ahmed alisema wazazi wanapaswa kuwa na ufahamu wa walipo watoto wao wakati wote.

Hata imebainika kwamba wazazi wa wasichana wale wengine walio mikononi mwa watekaji nyara hawajapiga ripoti kwa maafisa wa kiutawala au polisi.

“Habari ambazo tumepokea ni kwamba kulikuwa na wasichana wengine wawili ambao walikuwa ndani ya gari hilo na hakuna mtu anajua waliko kwa sasa. Ni muhimu wazazi kuwa waangalifu hasa msimu huu ambapo watoto wako nyumbani. Ofisi yangu ilizungumza na OCPD wa Kaunti na tumeanza uchunguzi tayari,” akasema Bw Ahmed.