Moi alikuwa amejiandaa kuondoka duniani – Askofu
Na WANDERI KAMAU
RAIS Mstaafu Daniel Moi alikuwa amejitayarisha kwa safari yake ya mwisho duniani, amesema Askofu Mstaafu Silas Yego wa kanisa la African Inland Church (AIC).
Akikumbuka mazungumzo yao ya mwisho, askofu huyo alisema kuwa Mzee Moi alimwambia kwamba siku zake za mwisho duniani zilikuwa zimekaribia, na alikuwa amejitayarisha.
“Mnamo Septemba 5, mwaka uliopita, familia ya Mzee Moi ilifanya kikao maalum kujuliana hali. Nilialikwa kwenye kikao hicho. Baadaye, Mzee [Moi] alinialika ambapo tulifanya mazungumzo maalum kuhusu safari yake ya Kikristo. Aliniambia amejitayarisha kuondoka,” akasema.
Askofu Yego ndiye aliongoza viongozi wengine wa kidini kutoa jumbe za kumsifu Mzee Moi kwenye mazishi yake yaliyofanyika nyumbani kwake, katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru.
Kutokana na hilo, alimwagiza kuhakikisha kuwa familia yake itaendelea kuzingatia maadili ya Kikristo hata atakapofariki.
Na ili kutimiza ombi la Mzee Moi, aliwapa wanawe Biblia kila mmoja, kama ishara ya kuhakikisha kwamba wanaendeleza neno la Mungu.
Vile vile, aliwasomea Kitabu cha Yoshua 1:8, kama alivyopendelea Mzee Moi kabla yake kuzikwa: “Wekeni kitabu hiki cha sheria rohoni mwenu; kitathmini mchana na usiku ili muwe makini mnapoyatimiza yale yaliyoandikwa. Kwa hayo, mtapata mafanikio maishani mwenu.”
Askofu pia aliwaomba wanasiasa kutumia nafasi na ushawishi wao kuendeleza umoja, kama alivyofanya Mzee Moi.
“Katika uhai wake wote, marehemu alitilia maanani umoja miongoni mwa Wakenya. Hilo ndilo lilikuwa tamanio lake daima. Hivyo, ombi langu kwa wanasiasa ni kuhakikisha kuwa hawatumii nafasi zao kuzua migawanyiko isiyofaa,” akasema.
Baadhi ya viongozi wakuu wa kidini waliokuwepo ni Kadinali John Njue wa Kanisa Katoliki, maaskofu Arthur Kitonga (Kanisa la Redeemed), Eliud Wabukala (mwenyekiti EACC), Jakson Ole Sapit (kanisa la ACK) kati ya wengine.
Askofu Kitonga alimsifu Mzee Moi kama kiongozi mkarimu, aliyeshiriki kwenye hafla nyingi za kuchangisha fedha za kujengea makanisa.
Alisema kuwa Mzee Moi hangesita kushiriki kwenye mialiko aliyopata ya kuchangisha fedha za kujengea kanisa.
Askofu Wabukala alimtaja kuwa kiongozi ambaye alizingatia maadili na Ukrito, licha ya kuwa mamlakani.