Morara Kebaso akamatwa tena kwa madai ya kuhusika katika fujo Bomas
MWANAHARAKATI wa kisiasa, Morara Kebaso, amekamatwa tena siku chache tu baada ya korti kumwondolea mashtaka alipokamatwa wiki mbili zilizopita.
Bw Morara alisema alikamatwa jana jijini Nairobi kuhusiana na vurugu zilizozuka Bomas of Kenya Ijumaa iliyopita, ambapo Wakenya walikusanyika kutoa maoni yao kuhusu pendekezo la kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Ripoti zinaashiria kuwa mwanaharakati huyo alichukuliwa na makachero waliokuwa na magari aina ya Subaru waliompeleka katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata kumhoji.
“Nimekamatwa kuhusu kilichotokea Bomas. Hebu tafakari hayo? Hii ni nini sasa,” aliandika katika mtandao wa kijamii wa X.
Saa moja kabla ya kukamatwa, mwanaharakati huyo alikuwa amekashifu kitendo cha kumteka nyara afisa wa mawasiliano ya kidijitali katika chama cha KANU, Cornelius Ronoh, Jumatatu jioni katika eneo la Fedha, Embakasi.
“Uhuru wa kujieleza tunaofurahia sio zawadi kutoka kwa serikali, ni haki. Kutekwa nyara kwa mtindo wa kihuni kwa Cornelius Ronoh kunaonyesha jinsi serikali inavyochukia ukweli. Acha niwahakikishie jambo moja, tutaongea ukweli bila woga. Kenya ni nyumbani. Hamtakuwa serikalini milele,” alichapisha.
Tukio hilo la kumkamata jana limejiri siku nne baada ya Morara kushambuliwa kikatili alipofika Bomas of Kenya kutoa maoni yake na alionekana kuwa katika hali mbaya familia yake ilipotoa hotuba kuelezea wasiwasi kuhusu usalama wake Jumapili iliyopita.
Msemaji wa familia hiyo Tom Moindi alilaani shambulizi hilo na kusihi serikali kuwapa wanaharakati ulinzi wa polisi.
Morara alikamatwa huku waliomteka nyara Bw Ronoh wakimwachilia huru katika Kaunti ya Kiambu baada ya kumzuilia usiku wote katika “nyumba ya siri.”
Katika mahojiano na Taifa Leo, afisa huyo wa mawasiliano alisema aliachwa Kiambu Road karibu na Jumba la Kibiashara la Ridgeways, jana asubuhi.
Alisema waliomteka nyara, anaowashuku kuwa maafisa wa polisi walimhoji kuhusu mchakato wa kumtimua Bw Gachagua na jumbe zake mitandaoni kuhusu suala hilo.
Katika jumbe hizo zenye anwani#KufaDerevaKufaMakanga Bw Rono alipigia debe kuondolewa kwa Bw Gachagua na bosi wake, Rais William Ruto.