Habari Mseto

Moto: Wafanyakazi wa juakali wakadiria hasara Viwandani

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

WAFANYAKAZI katika barabara ya Kitui kwenye Eneo la Viwandani, Kaunti ya Nairobi wanakadiria hasara ya Sh1.5 milioni baada ya moto kuteketeza mali usiku wa kuamkia Jumatano.

Kwa mujibu wa Bw Muoka Mutuku, ambaye hufanya biashara ya kuyeyusha vyuma, moto ulianza mwendo wa saa sita na nusu za usiku.

Moto waharibu mali Viwandani, Nairobi. Picha/ Sammy Kimatu

“Nilipigiwa simu na mlinzi kwamba moto umetokea kazini. Nilienda hadi kwa kituo cha zimamoto kilicho karibu na mtaa wa Mukuru-Kaiyaba na ndiposa waliharakisha na kwenda kuuzima,” akasema Bw Mutuku.

Kando na karakana yake, kioski cha M-pesa, stoo ya vipuri vya magari na mashine za juakali pamoja na hoteli mbili ziliteketea pia.

“Jokovu langu jipya lilibakia kuwa majivu. Chakula na fanicha pia viliteketea,” Bi Ida Mashaka akaeleza.

Karibu na palipochomeka kuna gereji mbili kubwa ambamo moto haukufika. Magari ya watu binafsi yalikiuwa yameegeshwa pahali hapo.