Habari Mseto

Motoni kwa kudai wana uwezo wa kupima corona

March 18th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kliniki Nairobi alishtakiwa Jumanne kwa kutangaza habari za uwongo katika mitandao ya kijamii kuwa alikuwa na kifaa cha kupima virusi vya corona.

Dkt Pravan Mehendra Pancholi, mmiliki wa kiliniki ya Avane kilichoko Yaya Centre pamoja na mfanya kazi wake Sylvia Ndinda Kaleve alishtakiwa mbele ya hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe.

Katika kiliniki yake , Dkt Pancholi huwafanyia upasuaji wale wanaotaka kubadili maumbile ya ngozi na wanawake wanaotaka kuongezewa viuno!

Kufuatia agizo la Jaji Mkuu David Maraga mahakama zifungwe kufuatia kuzuka kwa maradhi ya Covid-19 ilibidi kesi dhidi ya Dkt Pancholi na Bi Kaleve isikizwe hadharani.

Bi Nzibe alisikiza kesi hiyo katika eneo la kuegesha magari katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Kiti na meza ya hakimu ikiwa katika egesho la magari mahakama ya Milimani. Picha/ Richard Munguti

Dkt Pancholi na Bi Kaleve walikanusha mashtaka matatu ya kutangaza katika mitandao ya kijamii kwamba walikuwa na vifaa vya kupima virusi vya corona.

Dkt Pancholi alishtakiwa kosa la kutoa huduma za kiliniki bila kukisajili katika bodi inayothibiti hospitali.

Bi Kaleve alikabiliwa na shtaka la kutekeleza majukumu ya daktari akiwa hajahitimu.

Wawili hao walikanusha kutoa huduma hizo mnamo Machi 16, 2020 katika kiliki cha Avane kilichoko Yaya Centre eneo la Kilimani kaunti ya Nairobi.

Viongozi wawili wa mashtaka waliomwakilisha Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Joseph Gitonga Riungu na Bi Jacinta Nyamosi walipinga wawili hao wakiachiliwa kwa dhamana wakisema “walitaka kuwalaghai Wakenya wakidai walikuwa na kifaa cha kupima virusi vya corona.”

Bw Gitonga alisema tayari shirika la afya ulimwenguni (WHO) limetangaza ugonjwa huu kuwa janga la kimataifa na kwamba “Dkt Pancholi alikuwa na nia ya kuwalaghai Wakenya kwa kutangaza katika mitandao ya kijamii kwamba alikuwa na kifaa cha kupima virusi vya corona.”

“Kwa kujali afya ya Wakenya wote Rais Uhuru Kenyatta amechukua tahadhari na kuamuru wizara ya afya ifanye juu chini kuhakikisha wananchi hawajaathiriwa na ugonjwa huu ulioanzia nchini Uchina,” alisema Bi Nyamosi.

Hakimu alifahamishwa washtakiwa hawa kwa kuongozwa na tamaa waliweka matangazo kwamba “kumesalia vifaa 400 tu kati ya 1,000 walizokuwa nazo na umma unahimizwa kuharakisha kununua kabla havijaisha.”

Hakimu mkazi Caroline Muthoni Nzibe. Picha/ Richard Munguti

Bw Gitonga alisema washtakiwa walikuwa wametoa nambari ya Mpesa ya kulipia vifaa hivyo.

“Naomba hii mahakama iwanyime dhamana kwa vile watavuruga uchunguzi na mashahidi,” alisema Bw Riungu.

Mahakama iliombwa itilie maanani tayari wananchi wameshtushwa na ugonjwa huu na wangelianza kumiminika katika kiliniki cha Dkt Pancholi kununua vifaa hivi.

Lakini wakili Stanley Kang’ahi aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana washtakiwa akisema ,” hakuna ushahidi uliowasilishwa jinsi washtakiwa watakavyovuruga uchunguzi na mashahidi.”

Alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa na kwamba “wawili hao wanastahili kuachiliwa kwa masharti.”

Viongozi wa mashtaka Gitonga Riungu na Jacinta Nyamosi. Picha/ Richard Munguti

Bw Kang’ahi alisema tayari wizara ya Afya imefunga kiliniki cha Dkt Panchori na wafanyakazi zaidi ya 30 kutimuliwa.

“Kiliniki cha Dkt Panchori kimesajiliwa na Serikali na madai hakijasajiliwa yanapotosha,” Bw Kang’ahi.

Wakili huyo aliomba washukiwa hao waachiliwe kwa dhamana.

Hakimu aliwaachilia wawili hao kwa dhamana ya Sh150,000 kila mmoja hadi Aprili 20 kesi itakapotajwa kwa maagizo zaidi.

Bi Nzibe alikataa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwamba “washtakiwa hao watawavuruga mashahidi na uchunguzi. “