Habari Mseto

Mpango kusambaza vyakula kupunguza visa vya wanafunzi kuacha shule

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

WANAFUNZI wa shule za upili za kutwa eneo la Keiyo Kusini, wamepata afueni baada ya kushirika kujitolea kuwapa chakula cha mchana kwa lengo la kupunguza ongezeko la visa vya kuacha shule.

Mpango huo umefanikishwa na Child Welfare Society of Kenya kwa ushirikiano na afisi ya mbunge wa eneo hilo.

Kulingana na shirika hilo la kushughulikia maslahi ya watoto nchini, mpango huo unaenda sambamba na sera ya serikali kuhakikisha mpito wa asilimia 100 kwa 100 wanafunzi wanajiunga na shule za upili.

Ukilenga wanafunzi 6, 000, hata hivyo, utanufaisha shule za upili za kutwa Keiyo Kusini.

Ulizinduliwa wikendi kupitia ushirikiano kati ya shirika hilo na mbunge wa eneo hilo Gideon Kimaiyo, ukitazamiwa kusaidia shule 26 za upili za umma.

“Leo tumezindua usambazaji wa vyakula na vitabu kwa shule za upili Keiyo Kusini, na tunatumai wanafunzi watapata motisha kukata kiu cha masomo,” alisema Mwakilishi wa Shirika hilo, Bi Tafroza Shunza.

Msaada wa vyakula vilivyotolewa ni pamoja na mchele,mahindi, mafuta ya kupikia.

Uzinduzi huo ulifanyika katika Shule ya Sekondari ya Kapchorwa.

Bi Shunza alisema walianza mpango wa chakula shuleni ili kusaidia kupunguza visa vya watoto kutoka jamii maskini kuacha shule.

“Mwaka jana (2023) tulikuwa tukitoa chakula cha mchana kwa watahiniwa, lakini baada ya kuona jinsi watoto walivyokuwa wakiteseka tuliamua kupanua mawazo zaidi; kuwapa watoto wote chakula,” alisema Bi Shunza, akisikitikia kero ya watoto kuacha shule kwa sababu ya njaa.

Afisa huyo alielezea imani yake kuwa mkondo huo utasaidia kuboresha kiwango cha masomo Keiyo Kusini.

Aidha, shirika hilo limeanzisha mpango sawia na huo katika kaunti mbalimbali, zikiwemo Murang’a, Kiambu na Baringo ambapo wanafunzi zaidi ya 25,000 wananufaika.