Habari Mseto

Mpango wa maridhiano una dosari, asema mwenyekiti wa chama cha wanafunzi vyuo vikuu vya kibinafsi nchini Kenya

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

MPANGO wa maridhiano (BBI) ni mwema kuiendesha Taifa la Kenya vizuri Ila una dosari.

Alizungumza Jumatano, mwenyekiti wa Chama Cha Wanafunzi Vyuoni Vikuu vya Kibinafsi Nchini Kenya (KPUSA), Bw Brian Amollo alisema ni makosa rais kuwa na nguvu nyingi alisema hilo ni hatari na huenda taasisi nyingi zikakandamizwa.

Badala yake, Bw Amollo alisisitiza ni vyema Uhuru wa taasisi za idara za serikali kuheshimiwa.

Aidha, aliomba serikali kusambaza nakala za stakabadhi hiyo kwa wanachi kutoka jijini hadi mijini na mashambani ndiposa wakenya wajisomee.

“Kuna pia umuhimu wa wakenya kuhamasishwa kuhusu BBI kisha kila mkenya apate nakala yake,” akasema.

Zaidi ya hayo, aliikosoa serikali akisema uchumi wa Taifa umezorota ilhali serikali inatumia mabilioni ya pesa juu ya BBI.

“Uchumi wa Kenya uko chini mno ilhali serikali inatumia mabilioni ya pesa kwa BBI huku wakenya wakikosa kazi na kulala njaa,”” Bw Amollo akaambia Taifa Leo.

Kadhalika, Bw Amollo aliwakashifu viongozi wa siasa kwa kuongoza mikutano mikubwa na kuonya kwamba hii ni hatari kwa kusababisha msambao wa virusi vya corona.

Alimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuzima mikutano yote ya hadhara sawia na kupunguza saa za kufungua baa na kuongeza kafyu hadi 2021. Vilevile, Bw Amollo aliitaka serikali kutoa ripoti ya tume zote ikiwemo ya Waki miongoni mwa tume zingine ndiposa Wakenya wajue ukweli na kuwa na imani na serikali yao.

“Ni vyema kwa wakenya kuambiwa ukweli kuhusu ripoti za tume zote zilizoteuliwa kushughulikia masuala.mbalimbali ya kitaifa ikiwemo ripoti ya Waki na zinginezo ili wakenya wawe na imani na serikali yao,” Bw Amollo adokeza.