Mradi wa filamu watazamiwa kuiletea Fort Jesus Sh20 bilioni
Na DIANA MUTHEU
KWA miaka 10 ijayo, ngome ya Fort Jesus na mji wa Old Town, Kaunti ya Mombasa zitaweza kufanyiwa ukarabati ambao utazisaidia kurejesha hadhi yao ya zamani.
Hii ni baada ya uongozi wa Fort Jesus kushirikiana na kampuni moja ya kutoa huduma za teknolojia ya Jays Pyrotechnics Ltd kufanya maonyesho ya historia ya ngome hiyo, ambayo yatakuwa yakionyeshwa kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Jays Pyrotechnics Ltd, Bi Jayshree Suchak, kwa muda wa miaka kumi hivi wanatazamia kupata mapato ya Sh20 bilioni kutoka kwa mradi huo.
“Fedha hizo zitatumika kukarabati ngome hii na mji wa Old Town ili kuirejeshea hadhi yake ya zamani,” akasema Bi Suchak.
Alisema kuwa mradi huo wa kutengeneza picha na kutumia teknolojia kuelezea matukio ya kale uliwagharimu Sh150 milioni na uliwachukua muda wa miaka miwili toka 2018 hadi 2020.
Utafiti na utengenezaji wa filamu na picha hizo ulifanywa na Wakenya. Jumatano jioni, picha hizo zilionyeshwa katika ukuta mmoja wa ngome hiyo kupitia teknolojia ya sasa maarufu kama “Augmented Reality”.
Bi Suchak alisema mradi huo utawasaidia kueleza Wakenya na wageni kuhusu historia ya ngome hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 400.
Kulingana na Waziri wa Michezo na Turathi za Kitaifa, Dkt Amina Mohamed, mradi huo ni muhimu sana kwa kuwa unaelezea historia ya nchi yetu.
Dkt Amina alisema kuwa mradi huo ni moja kati ya maendeleo katika mpango unaojulikana kama “People of Kenya” (watu wa Kenya)- Utamaduni wetu, wa kuwatafuta na kufuatilia historia ya mashujaa wa humu nchini, uliozinduliwa katika makavazi ya Nairobi hivi majuzi.
“Mradi huo utatusaidia kujivunia historia ya mahali tumetoka kama nchi. Pia, itatusaidia kukubali mazuri na mabaya yaliyotokea hapo kale, kwani yote ni hatua tofauti katika historia yetu na tutazisherehekea kwa njia tofauti,” akasema Dkt Amina.
Katika eneo la Pwani, kuna maeneo tofauti ya kihistoria kama vile mnara wa Vasco Da Gama, mabaki ya Gedi Ruins na mengineyo ambayo bado yanahitaji kuhifadhiwa kwa manufaa ya watalii.
“Tumeanza kukarabati baadhi ya majengo haya ya zamani huku tukivumbua mengine. Kila eneo la kihistoria litakarabatiwa,” akasema waziri.