Mradi wa Talanta na Kazi walenga kuwainua vijana
Na MAGDALENE WANJA
KILA mwaka, maelfu ya wanafunzi hufuzu kutoka kwa vyuo vikuu mbalimbali nchini huku nafasi za kazi zikiendelea kuwa adimu nchini.
Wengi hupitia madhila na mfadhaiko wanapokosa nafasi za kazi na huingilia utumizi wa mihadarati na uhalifu kama shughuli yao ya kila siku.
Ni kwa sababu hii shirika la Sarakasi Trust limeanzisha mpango wa kutumia sanaa kuwapa vijana nafasi za kazi katika kaunti za Mombasa na Kilifi.
Mradi huo kwa jina Talanta na Kazi umefadhiliwa na ubalozi wa Amerika.
“Nia yetu ni kuwapa vijana nafasi ya kujitegemea maishani ili kuwafanya waweze kuzifanya talanta zao kuwa biashara ambazo watazitegemea pamoja na jamii zao,” alisema msimamizi wa mradi huo Bi Anita Mbugua.
Vijana kujitegemea
Alisema kuwa nia yao ni kuwafanya vijana 500 kujitegemea baada ya kupokea mafunzo hayo ambayo yatachukua muda wa mwaka mmoja.
“Tunawatafuta vijana 500 ambao watapokea mafunzo hayo wakiwemo 250 wa Kilifi na 250 kutoka kaunti ya Mombasa,” alisema Bi Mbugua.
Mafunzo watakayopokea ni pamoja na ujuzi katika maswala ya uongoz.
“Tungetaka pia kuwaunganisha na baadhi ya wasanii ambao wamefaulu katika kutumia vipaji vyao na kuvigeuza fursa za kibiashara,” aliongeza Bi Mbugua.