Habari Mseto

Msaada wa Rais wa Sh10,000 uko wapi? ODM sasa wauliza

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WINNIE ONYANDO

VIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wanadai kuwa serikali ya Kenya Kwanza haijatimiza ahadi yake ya kutoa msaada wa Sh10,000 kwa waathiriwa wa mafuriko hasa wale ambao walipoteza makazi yao.

Wakiongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, viongozi hao walisema kuwa serikali ya Rais William Ruto ilitoa ahadi hewa huku wahasiriwa wa mafuriko, hasa wale ambao nyumba zao zilibomolewa, wakiendelea kuteseka.

“Rais William Ruto aliahidi kuwalipa wale ambao nyumba zao zilibomolewa Sh10,000. Ahadi hiyo haijatekelezwa,” akasema Bw Sifuna.
Mbali na hayo, viongozi hao walidai kuwa serikali inafaa kuwapa wahasiriwa angalau Sh20,000 kwani hiyo Sh10,000 haitoshi.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza Alhamisi jijini Nairobi baada ya kupokea misaada tofauti kutoka kwa viongozi mbalimbali nchini.

Misaada hiyo inalenga kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko.

Hata hivyo, Taifa Leo ilipozungumza na Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura kupitia njia ya simu, Bw Mwaura alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa shughuli za kutoa msaada huo zinaendelea.

Bw Mwaura alieleza kuwa kati ya Mei 17 na 18 mwaka huu, serikali ilituma Sh10,000 kwa familia 9,972.

“Mpango huo unaendelea na kufikia sasa, jumla ya familia 9,972 zimepokea pesa hizo. Mbali na hayo, tunalenga familia 40,000 na kufikia sasa tuna data kamili ya familia 26,000,” akasema Bw Mwaura.

Alisema kwamba pesa hizo zinatumwa kupitia M-pesa.

Mnamo Mei 6, Rais Ruto alisema kila familia kati ya 40,000 zilizohamishwa na mafuriko itapokea msaada wa Sh10,000.

Akizungumza alipowatembelea waathiriwa wa mafuriko katika mtaa wa Mathare, Dkt Ruto alizihakikishia familia ambazo nyumba zao zilibomolewa kuwa zitapewa eneo mbadala la kuishi hadi shughuli hiyo itakapokamilika.

“Kwa familia zote 40,000 ambazo zimehamishwa kwa sababu ya usalama wao, serikali itatoa Sh10,000 kwa kila familia kutafuta makazi mbadala ya muda hadi pale itakapoelekezwa na serikali,” alisema.