• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
Msajili wa vyama akataa ‘Jubilee Asili’ na ‘Hustler’

Msajili wa vyama akataa ‘Jubilee Asili’ na ‘Hustler’

Na LEONARD ONYANGO

MSAJILI wa Vyama vya Kisiasa amekataa maombi ya kusajili ‘Jubilee Asili’ na ‘Hustler’ kama vyama vya kisiasa huku akisema kuwa majina hayo yanakiuka sheria.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu alisema Jumanne kuwa afisi yake imepokea zaidi ya maombi 20 ya kutaka kusajili Jubilee Asili na ‘Hustler’ kuwa vyama vya kisiasa tangu Februari 2020.

Naibu Rais Dkt William Ruto mnamo Juni 2020 alizindua afisi mbadala yenye jina Jubilee Asili Centre katika mtaa wa Kilimani jijini Nairobi na kuzua tetesi kuwa huenda alinuia kuunda chama kipya.

Wakati wa uzinduzi huo, Dkt Ruto alizindua kaulimbiu mpya ya ‘Sote Pamoja’ badala ya ‘Tuko Pamoja’ inayotumiwa na chama cha Jubilee.

Wandani wa Dkt Ruto wanashikilia kuwa walifungua afisi hiyo ya Jubilee Asili ili kupata ukumbi wa kukutana baada ya kufungiwa nje ya makao makuu ya chama cha Jubilee katika mtaa wa Pangani, Nairobi, kwa zaidi ya miezi saba.

Jana, Bi Nderitu aliambia Taifa Leo kuwa alikataa kusajili Jubilee Asili kuwa chama cha kisiasa kwa sababu jina hilo linakiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa ambayo inataka jina la chama kinachopendekezwa lisifanane au kukaribiana na chama kilichoko.

Kifungu cha 8(c) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa kinaruhusu Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa ombi la kusajili chama ikiwa jina lina matusi, na ama linafanana au kukaribiana na chama ambacho tayari kimesajiliwa.

“Vyama vya Jubilee Asili na Jubilee vinaweza kukanganya wapigakura wakati wa uchaguzi. Hiyo ndiyo maana tumetupilia mbali maombi ya kukisajili chama cha Jubilee Asili,” akasema Bi Nderitu.

Inaonekana Dkt Ruto aliamua kuvamia makao makuu ya chama cha Jubilee wiki iliyopita baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuzima juhudi zake za kusajili Jubilee Asili.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa pia alisema kuwa alikataa kusajili ‘Hustler’ kuwa chama cha kisiasa kwa sababu kinaendeleza ubaguzi kinyume na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011.

Dkt Ruto amekuwa akijiita ‘hustler’ (mlalahoi) kwa lengo la kujitafutia ufuasi miongoni mwa Wakenya maskini huku akijiandaa kuwania urais 2022.

Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa vigogo wakuu serikalini wamekataa kumuunga mkono kuwa rais mwaka wa 2022 kwa sababu yeye ni mtoto wa maskini.

“Tukisajili Hustler inamaanisha kitakuwa chama cha walala-hoi. Hivyo, kuna uwezekano wa watu wenye uwezo wa kipato kutokubaliwa kujiunga na chama hicho. Huo ni ubaguzi wa watu kwa misingi ya matabaka,” Bi Nderitu akasema.

“Kifungu cha 6(d) kuhusu maadili ya vyama kinataka vyama vya kisiasa kuhakikisha kuwa havibagui watu kwa misingi ya matabaka ya kiuchumi, kikabila, jinsia na kadhalika,” akasema.

Bi Nderitu, hata hivyo, alisema kuwa hajui ikiwa waliotuma maombi ya kusajili Jubilee Asili na Hustler kuwa vyama vya kisiasa walifanya hivyo kwa niaba ya Naibu wa Rais au la.

Mara nyingi wanasiasa wakuu hutumia watu wasiojulikana kusajili vyama vyao.

Jumla ya vyama 71 vimesajiliwa kuwa vyama vya kisiasa humu nchini. Vyama 10 vimeidhinishwa kuanza mikakati ya kutafuta wanachama kutoka angalau kaunti 24 kabla ya kusajiliwa.

Chama kilichoidhinishwa hivi karibuni kuanza kutafuta wanachama ni Mabadiliko Party of Kenya ambacho kilipewa idhini Septemba 21, mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

Kesi ya pili ya Sonko yaanza kusikizwa faraghani

Trump ‘ashindwa kupumua’ baada ya kurudi White House