Habari Mseto

Msako wa lori lililoangamiza ‘Tiktoka’ Brian Chira

March 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

POLISI wameanza msako dhidi ya lori ndogo linalodaiwa kumgonga na kumuua ‘Tiktoka’ maarufu Brian Chira mnamo Jumamosi, Machi 16, 2024 alfajiri.

Chira alipoteza maisha papo hapo baada ya kugongwa na lori hilo, katika eneo la Karuri, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na polisi, ajali hiyo ilifanyika katika barabara ya Ruaka-Ndenderu, mwendo wa saa tisa alfajiri Jumamosi.

Lori hilo ndogo lenye rangi nyeupe halikusimama baada ya kumgonga barobaro huyo maarufu kwenye mitandao ya kijamii.

Polisi wamesema kuwa kuna mipango ya mwili huo kufanyiwa upasuaji kama sehemu ya juhudi za uchunguzi.

Pia, wasemema kuwa wanapanga kwenda maeneo ambako marehemu alizuru kabla ya ajali hiyo kufanyika.

Polisi wanachunguza kubaini madai kwamba marehemu alikuwa mlevi wakati ajali hiyo ilipotokea katika eneo la Gacharage.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Kiambaa, Bw Pius Mwanthi, alisema kuwa bado hawajafanikiwa kupata lori lililomgonga kijana huyo.

“Ajali hiyo ilifanyika nyakati za usiku. Kwa sasa, juhudi zinaendelea kusaka gari lililohusika. Hatujakamata mtu yeyote kufikia sasa,” akasema.

Alisema polisi watazichunguza kamera za barabarani zilizo karibu na eneo hilo kama njia za kujaribu kutambua lori hilo.

“Dereva aliyehusika anafaa kujitokeza na kuripoti tukio hilo, ili kutusaidia kwenye shughuli za uchunguzi,” akasema.

Chira alikuwa akipelekwa nyumbani kwao na rafikiye kwa pikipiki wakati ajaji hiyo ilipofanyika.

Mmoja wa marafiki wake alisema alimchukua nje ya kilabu moja katika eneo hilo, baada ya kufurushwa nje na walinzi kwa madai ya kuzua vurugu.

Walioshuhudia walisema alikuwa mlevi kupindukia, hali iliyofanya walinzi kumtoa nje. Kilabu hiyo pia ilikuwa ikikaribiaa kufungwa.

Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya City, ukingoja kufanyiwa upasuaji.