Habari Mseto

Mshtakiwa wa wizi wa mbolea augua

January 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

KUSIKILIZWA kwa kesi inayomkabili mkulima kutoka Narok anayeshtakiwa kuhifadhi magunia 252 ya mbolea ya bei nafuu akijua imeibwa, kulitibuka Ijumaa alipougua akiwa rumande.

Kufuatia kuugua kwa Bw Raphael Kipng’etich Bett almaarufu ‘Wifi’ akiwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill, Nairobi, hakimu mkuu mahakama ya Milimani, Nairobi Lucas Onyina aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitalini.

Na wakati huo huo, Bw Onyina alitenga kesi hiyo itajwe Januari 9, 2024, kutengewa siku nyingine ya kusikilizwa.

Pia hakimu aliamuru upande wa mashtaka uandae ushahidi wote na kumkabidhi mshtakiwa.

Kusikilizwa kwa kesi hiyo kuliahirishwa ghafla, punde tu polisi walipotandaza magunia yenye mbolea hiyo katika egesho la magari katika mahakama ya Milimani wakisubiri Bw Onyina aikague.

Kiongozi wa mashtaka aliomba hakimu aikague mbolea hiyo ndipo ipelekwe kuhifadhiwa katika mabohari ya halmashauri ya nafaka na mazao (NCPB) ambako hakuna unyevu unyevu.

Wakili Kennedy Ayambei alipinga kesi dhidi ya Bw Bett ikianza kusikizwa licha ya mbolea kutandazwa nje akisema “ni mgonjwa na hatakuwa na makini kufuata ushahidi ukitolewa.”

Pia wakili huyo alisema mnamo Alhamisi alipewa nakala za mashahidi wanne lakini amekabidhiwa barua nyingine Ijumaa asubuhi ishara kwamba uchunguzi unaendelea.

Bw Ayambei aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi pale polisi watakuwa wamekamilisha uchunguzi.

  inayotolewa kwa wakuliman wa mashamba madogo na makubwa nchini.

Bw Bett almaarufu “Wifi” alishtakiwa mbili baada ya mkulima mwingine Hilary Samoei kushtakiwa kwa kuilaghai serikali magunia 2,398 ya mbole yenye thamani ya Sh7,063,000.

Bw Bett alikanusha shtaka la kupatikana akiwa na magunia 252 ya mbolea yenye thamani ya Sh630,000 mnamo Januari 2,2024 katika eneo la Olololungah Narok kusini.

Hakimu alielezwa mshtakiwa alikamatwa na Konstebo Ronald Chemosit na Konstebo Norman Mwakawa kutoka kitengo maalum cha kupambana na jinai (DCI).

Mshtakiwa huyo alikana shtaka kisha kiongozi wa mashtaka akaomba hakimu arodheshe kesi hiyo isikizwe leo (Ijumaa) kuokoa mbolea hiyo isiharibike.

“Mbolea ni miongoni mwa bidhaa zinazoharibika upesi.Naomba hii mahakama itenge kesi hii isikizwe kwa upesi kabla yah ii mbolea kuharibika,” kiongozi wa mashtaka alifafanua.

Hakimu alielezwa mbolea hii inatakiwa kuhifadhiwa katika bohari la halmashauri ya nafaka na mazao (NCPB) ikisubiri kupewa wakulima Machi 2024.

“Hii mbolea inatakiwa kupewa wakulima kabla ya mvua ya Masika,” kiongozi wa mashtaka aliambia korti.

Bw Ayambei aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akashughulikie jinsi watoto wake watakavyorudi shule.

“Mshtakiwa hana mapato makubwa. Naomba korti imwachilie kwa dhamana ya chini,” Bw Ayambei alidokeza.

Hakimu alifahamishwa watu wa familia ya mshtakiwa wanaweza kupata tu Sh50,000 ambazo wanaweza kulipa kama dhamana mshtakiwa atoke gerezani.

Lakini Bw Onyina alikataa maelezo hayo na kuamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu ama dhamana sawa na hiyo.

Samoei aliyeshtakiwa kwa ulaghai wa mbolea magunia 2,398 yenye thamani ya Sh7,063,000 aliachiliwa pia kwa dhamana ya Sh500,000 baada ya kueleza mahakama mkewe alijifungua mapacha mnamo Desemba 30, 2023.

Bw Samoei alieleza mahakama ndiye anasubiriwa kumlipia mkewe bili ya hospitali ndipo aruhusiwe kuenda nyumbani kuanza kazi ya kuwalea wanawe.