Habari Mseto

Mshukiwa alaani kesi ya Waititu kuvuruga harusi yake

July 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MMOJA wa washukiwa 12 wanaoshtakiwa pamoja na gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ‘Baba Yao’ kwa kashfa ya Sh588 milioni atakayefunga pingu za maisha Jumamosi ijayo (Agosti 3) ameeleza wasiwasi iwapo mipango yake itaendelea akipewa dhamana ya juu.

Samuel Muigai Mugo alisema ana hofu arusi yake itavurugika iwapo mahakama haitamwachilia kwa dhamana ya kiwango cha chini.

Bw Samuel Muigai Mugo alimweleza hakimu mkuu Lawrence Mugambi amwachilie kwa kiwango kidogo cha dhamana “ndipo aweze kufunga ndoa na kipenzi chake Lillian Wambui.”

Bw Mugo alieleza mahakama mshahara wake ni Sh124,000 na “hawezi kupata dhamana ya juu.”

Bw Mugo ameshtakiwa kwa kutofuata sheria za utoaji zabuni.

Ameshtakiwa pamoja na wanachama wengine wa kamati hiyo ya ukadiriaji kandarasi Zacharia Njenga Mbugua, Joyce Ngina Musyoka, Simon Kabocho Kang’ethe na Anslem Gachukia Wanjiku.

Kadi ya mwaliko wa harusi ya Bw Samuel Muigai na Lillian Wambui iliyowasilishwa kortini kama ushahidi kuwa Bw Muigai si fukara. Picha/ Richard Munguti

“Mshtakiwa sio fukara jinsi anavyotaka hii mahakama imchukulie,” alisema kiongozi wa mashtaka Vincent Monda huku akiisomea mahakama kadi ya mwaliko wa harusi.

Bw Monda alisema, “Mshtakiwa amewaalika wageni kwa sherehe ya kukata na shoka baada ya kufunga ndoa katika kanisa la PCEA JKMC Nderi. Karamu kuu itaandaliwa Karlo Grounds (Fairlawns School).”

Bw Monda alisema karamu atakayowaandalia wageni ni ishara kwamba mshtakiwa hana ufukara kama anavyotaka hii mahakama iamini.

Lakini wakili ProfTom Ojienda alisema mshtakiwa alisaidiwa na marafiki kuandaa harusi yake.

“Mshtakiwa aliachangiwa harambee na marafiki kuandaa arusi hii itakayofungwa Agosti 3, 2019.”

Prof Ojienda alisema makosa ya Bw Mugo na wenzake waliyofanya ni kutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kuidhinisha kandarasi kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited ya ujenzi wa barabara.

Mahakama ilifahamishwa kuwa makosa dhidi ya mshtakiwa huyo na wenzake wanne ni mabaya kwa vile ndiyo yalipelekea mamia ya mamilioni ya pesa kutoweka.

Bw Mugo na wenzake walizuiliwa katika kituo cha Polisi cha Kilimani hadi leo mahakama itakapoamua iwapo itawaachilia kwa dhamana au la.