• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mshukiwa wa pili katika mauaji ya bwanyenye Tob Cohen aachiliwa kwa dhamana

Mshukiwa wa pili katika mauaji ya bwanyenye Tob Cohen aachiliwa kwa dhamana

Na RICHARD MUNGUTI

BAADA ya kukaa rumande siku 49 mshukiwa wa pili katika kesi ya mauaji ya bwanyenye Tob Cohen, Peter Karanja ameachiliwa kwa dhamana Jumanne ya Sh4 milioni na wadhamini wawili wa Sh2 milioni kila mmoja.

Endapo atashindwa kupata dhamana hiyo, Peter Karanja, aliamriwa na Jaji Paul Ogembo alipe dhamana ya pesa taslimu Sh2 milioni.

Karanja, Jaji Ogembo alifahamishwa, kesi inayomkabili itaunganishwa na nyingine ambapo mkewe Cohen, Sarah Wairimu Kamotho ameshtakiwa.

Akimwachilia kwa dhamana, Jaji Ogembo amesema ijapokuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP kupitia viongozi wa mashtaka Catherine Mwaniki na Wangui Gichuhi walisema adhabu ya kesi dhidi ya Karanja ni kifo, “ hiyo sio sababu tosha kumwezesha kumnyima dhamana mshtakiwa.”

Jaji huyo amesema DPP alishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha kwamba mshtakiwa atatoroka akiachiliwa kwa dhamana.

Mahakama imesema mshukiwa anaweza kunyimwa dhamana iwapo kuna sababu tosha.

“DPP alitegemea madai kwamba kesi inayomkabili mshtakiwa ni mbaya na adhabu yake ni kifo endapo akipatikana na hatia,” amesema Jaji Ogembo.

Ameongeza kusema kuwa mshtakiwa anaweza kutoroka kwa kuhofia atatiwa kamba akipatikana na hatia.

Jaji Ogembo ameombwa na DPP amnyime dhamana mshtakiwa kwa vile hana makazi maalum na akiachiliwa kwa dhamana kisha akose kufika kortini polisi hawajui watamtoa wapi.

Akitoa uamuzi, Jaji Ogembo ametupilia mbali hayo ya DPP akisema “ hayana mashiko kisheria kumwezesha kumnyima mshtakiwa dhamana.”

Kuhakikisha mshtakiwa amefika kortini akiachiliwa kwa dhamana, Jaji Ogembo amemwamuru mshtakiwa awasilishe paspoti yake kortini.

Amemwagiza vilevile asithubutu kuwazugumzia mashahidi katika kesi hii.

Pia ameamriwa asiende katika makazi ya Cohen na ikiwa itabidi aende huko basi aombe idhini ya mahakama.

“Makazi ya Cohen yanalindwa na Polisi na ni mojawapo ya ushahidi utakaotegemewa katika kesi hii,” amesema Jaji Ogembo.

Jaji huyo amesema kuwa kifungu nambari 49 cha katiba kimeipa mahakama mamlaka ya kuwaachilia kwa dhamana washukiwa wanaofunguliwa mashtaka na Serikali.

Jaji Ogembo ametupilia mbali ombi la DPP kwamba Karanja anyimwe dhamana hadi kesi anayoshtakiwa pamoja na Sarah Wairimu Kamotho – mjane wa Cohen – isikizwe na kuamuliwa.

Karanja ameachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni na wadhamini wawili wa kiasi hicho wa Sh2 milioni kila mmoja.

Endapo atashindwa kupata dhamana hiyo ya Sh4m mshtakiwa ameagizwa alipe dhamana ya pesa taslimu Sh2 milioni.

Karanja amekanusha alimuua Cohen usiku wa Julai 19/20, 2019, akishirikiana na watu wengine.

Kesi itatajwa mbele ya Jaji Stellah Mutuku Novemba 12, 2019 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Raia wa Amerika kutuliza hasira gerezani

Waziri Matiang’i afungua KCPE kwa maombi

adminleo