Mshukiwa wa ubakaji wa Sudan Kusini kuona cha mtema kuni Uganda
Na RICHARD MUNGUTI
RAIA wa Sudan kusini alipelekwa nchini Uganda kushtakiwa kwa ubakaji baada ya kutorokea nchini Kenya Oktoba 12.
Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Muthoni Nzibe alifahamishwa kuwa Bw John Deng Garang ni miongoni mwa washukiwa wanaosakwa kwa ubakaji wa wanawake nchini Sudan kusini.
Bi Nzibe alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Ednah Ntabo kuwa Bw Garang alitoroka Sudan kusini na kuingia nchini Uganda.
“Naomba hii mahakama itilie maanani kuwa kumekuwa na visa vya wanawake kubakwa nchini Sudan kusini.Mshukiwa huyu ni mmoja wa wale wanaosakwa kwa uhalifu huo,” alisema Bi Ntabo.
Kiongozi huyo wa mashtaka alisema Bw Garang alijitambua kuwa mkimbizi kutoka Sudan kusini alipoingia nchini Kenya.
“Mshukiwa huyu ni miongoni mwa wale wanaosakwa kwa kuwabaka wanawake zaidi ya 150 Sudan kusini na Uganda,” Bi Ntabo alimweleza hakimu huku akiomba mkimbizi huyo apelekwe Ugada kujibu mashtaka
Bw John Deng Garang aliamriwa na hakimu mkazi Muthoni Nzibe akabidhiwe maafisa wa polisi wa kimataifa kusafirishwa hadi mahakama ya Kampala nchini Uganda kufunguliwa mashtaka ya ubakaji.
Bw Nzibe alisema kuwa mshukiwa huyo alitiwa nguvuni katika mtaa wa Shauri Moyo jijini Nairobi na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha uhalifu wa kimaeneo Bw Elijah Mabishi.
Mshtakiwa alitiwa nguvuni Novemba 22 na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri Nairobi.