Mshukiwa wa wizi wa pikipiki anusurika kifo kijijini Gakuo
NA GEORGE MUNENE
MSHUKIWA mmoja wa wizi wa pikipiki Jumamosi amenusurika kifo kwa tundu la sindano alipookolewa na polisi kutoka kwa umati wenye ghadhabu katika kijiji cha Gakuo, Kaunti ya Kirinyaga.
Mshukiwa huyo alipata majeraha mabaya alipovamiwa na kuchomwa moto na umati huo, lakini polisi waliingilia upesi na kumuokoa.
Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, ni kwamba inadaiwa mshukiwa aliiba pikipiki kutoka kwa mhudumu mmoja wa bodaboda katika mji wa Kutus na kuondoka nayo kuelekea Embu.
Hata hivyo, mwenye pikipiki hiyo alipiga kelele, na kuwavutia bodaboda wenzake waliofika na kumfuata mshukiwa ambaye alikamatwa katika kijiji cha Gakuo eneobunge la Mwea na kumshushia kichapo kwa marungu na mawe.
Walimuangusha na kumpiga kiberiti lakini polisi waliodokezewa tukio hilo, waliwahi upesi eneo hilo na kumuokoa.
Walioshuhudia walisimulia jinsi walivyowaona waendeshaji bodaboda hao wakimshika mshukiwa huyo na kumpiga, wakisema alikuwa miongoni mwa wahalifu kwenye genge lililokuwa likiiba mali yao eneo hilo.
“Tuliona waendeshaji hao wa bodaboda wakimkamata mwanamume huyo na kumshambulia. Nusura wamuue mshukiwa kabla ya maafisa wa usalama kuingilia kati,” akasema Bw Moses Mutugi.