Msichana aliyemuua mpenziwe kufanyiwa uchunguzi wa kiakili
NA FAUSTINE NGILA
Msichana aliyekisiwa kumuua mpenziwe Lang’ata, Nairobi Jumatano iliyopita atazuiliwa kwa siku tano zaidi ili afanyiwe uchunguzi wa kiakili.
Hakimu wa Kibera Estherb Boke aliwaruhusu polisi wamzuilie msichana huyo anayeaminika kuwa na miaka 12 kwenye kituo cha polisi cha Langa’ta ili kumaliza uchunguzi wa kifo cha kijana aliyefariki kwenye mitaa ya mabanda ya Lang’ata.
Polisi wamemzuilia msichana huyo anayeaminika kumdunga kisu mpenziwe wa kidato cha tatu huku wakisubiri mwili ufanyiwe upasuaji ili waweze kubaini kilichosababisha mauaji hayo.
Pia walisema kumzuilia msichana huyo kutamlinda dhidi ya wakazi ambao walikuwa tayari ‘kumtia adabu’ baada ya tukio hilo.
“Mshukiwa huyo alikamatwa na mwenyekiti wa Nyumba Kumi wa mtaa huo punde tu tukio hilo lilipotokea huku mwendazake akiwa na amedungwa visu viwili kifuani.
“Wakazi walikuwa wanataka kumkabili msichana huyo ambaye aliokolewa kwa kukamatwa na mwenyekiti wa Nyumba Kumi,” Susan Moracha alisema.
Alieleza kuwa kuna umuhimuwa wa kumzuia msichana huyo kutokana na kupigwa na wananchi waliokuwa wamejawa na ghadhabu.
Kulingana na polisi msichana huyo alikuwa amegombana na kijana huyo kabla ya kumdunga kisu.