Habari Mseto

Msichana skauti aliyeangamia ajalini azikwa

March 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

SIMANZI imetanda katika kijiji cha Gatundu wakati wa mazishi ya msichana skauti Shirleen Nyokabi Kariuki aliyeaga dunia Februari 25, 2024, katika ajali ya barabarani Kaunti ya Murang’a.

Shirleen aliaga dunia akiwa na umri wa miaka saba pekee, hali ambayo ilizidisha majonzi hasa wakiangalia picha yake ikiwa juu ya jeneza.

Shirleen alikuwa mmoja wa wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Maadili iliyoko Kaunti ya Kiambu walioaga dunia wakitoka Kaunti ya Nyeri kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya mwanzilishi wa vuguvugu la maskauti nchini Baden Powell.

Ajali hiyo ya saa moja jioni ilitokea wakati breki za basi la shule zilikataa kufanya kazi na likaanguka katika eneo la Mathioya.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang’a Kainga Mathiu alisema kwamba serikali katika eneo hilo haichukulii tukio hilo kama la kawaida.

“Kuna masuala nyeti ambayo tunapiga msasa kuhusu kujituma kwa wadau wote kuhakikisha usalama wa watoto. Tunataka kujua hali halisi ya basi hilo la shule, kama sheria za trafiki hasa kuhusu idadi ya abiria ilifuatwa, kwa nini maelekezo kwamba watoto wa shule wasisafirishwe usiku yalipuuzwa. Pia tutakagua hali ya kiafya ya dereva kujua ikiwa alikuwa amelewa au la,” akasema Bw Kainga.

Familia ya malaika Shirleen ikijumuika chini ya ‘Kariukis’, ilimweleza malaika Shirleen kama nuru ya maisha, ikisema alikuwa msichana mchangamfu.

Msichana skauti Shirleen Nyokabi aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka saba. PICHA | MWANGI MUIRURI

Katika risala za pamoja za familia hiyo, ilisema ilikuwa na matumaini makubwa kwa maisha ya msichana huyo ambaye kila siku werevu, tabasamu na mtazamo usio na ufisadi kwa maisha vilipamba maisha yake ya baraka.

Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata alifika katika mazishi hayo na akaeleza masikitiko yake kwa niaba ya serikali ya kaunti na wakazi.

“Letu ni kuwapa pole na kuwapa dua njema za watu wa Murang’a ambao kwa kauli moja wako na ninyi kwa maombi katika msiba huu,” akasema gavana Kang’ata.

Bw Kang’ata alisema kwamba serikali yake ilijizatiti kwa uwezo wake wote kushughulikia hali hiyo ya dharura.

Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata ahutubia waombolezaji katika misa kabla ya mazishi ya mwanafunzi skauti Shirleen Nyokabi. PICHA | MWANGI MUIRURI

Hii ni licha ya kwamba wazazi wa watoto hao 38 waliohusika katika ajali hiyo pamoja na walimu watatu na madereva wawili kulalamika kuhusu ukosefu wa uwezo thabiti wa kushughulikia dharura hiyo.

Akiungama nao, Bw Kang’ata alisema kwamba serikali yake iko na mpango wa kuzidisha uwezo wa kushughulikia dharura kupitia ujenzi wa wadi mpya katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Watoto wengine watano waliokuwa na majeraha mabaya zaidi katika wadi ya hali mahututi walihamishiwa katika hospitali nyingine.

Waombolezaji walioongea katika hali hiyo ya msiba mkuu walimsihi Mungu aondolee taifa la Kenya ajali za barabarani.

Aidha, walikemea matukio ya vifo vya watoto wadogo.