Msioe wasichana waliokeketwa, Njuri Ncheke waonya vijana
Na DAVID MUCHUI
Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke sasa linanuia kupiga marufuku kuolewa kwa wasichana waliopashwa tohara katika juhudi za kuimarisha vita dhidi ya ukeketaji.
Haya yalifichuliwa wakati wa mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Njuri Ncheke, Paul M’Ethingia katika mji wa Maua, Kaunti ya Meru, Jumatatu.
Marehemu M’Ethingia, mwenye umri wa miaka 81, kutoka Igembe Kusini alikuwa mwanaharakati mahiri wa kupinga ukeketaji (FGM) katika eneo hili ambalo utamaduni huo bado umekithiri.
Mwaka huu, visa kadhaa vya ukeketaji vimeripotiwa Kaunti ya Meru na Tharaka Nithi huku wilaya za Igembe North, Igembe Central, Tigania Central na Tharaka zikiongoza kwa visa vya kutahiri wasichana.
Wengine wengi wanasemekana kukeketwa kisiri.Katibu Mkuu wa Njuri Ncheke, Josphat Murangiri alisema viongozi wa baraza hilo wanapanga jinsi ya kutekeleza agizo hilo linalolenga kuangamiza ukeketaji.
Bw Murangiri alisema uamuzi huo ni sehemu ya juhudi za baraza la wazee za kuendeleza kazi ya marehemu M’Ethingia.
“Swali tunalojiuliza ni je, wasichana hawa wanatahiriwa kumnufaisha nani? Kwa nini tabia hii inaendelea hata baada ya Njuri Ncheke kupiga marufuku ukeketaji mnamo 1956? Kwa kuwa ni wanawake ambao hupasha tohara, wanaume sasa watachukua jukumu la kukataa uovu huu. Hatua tutakayochukua ni kuwaonya vijana wetu dhidi ya kuoa wasichana waliotahiriwa,” Bw Murangiri alisema.
Alisema wanawake na wanaume ambao wamekuwa wakiendeleza ukeketaji wanaona ni njia pekee ya kuwa na mke mwema akitaja imani hiyo kuwa potovu.
Mzee huyo wa Njuri Ncheke pia alilaumu wanaume wengine ambao wanaamini ukeketaji unaweza kusaidia wake zao kutulia katika ndoa.
‘Tunafahamu kwamba wanaume walioshindwa kutekeleza majukumu yao wanalazimisha wake zao kukeketwa. Tungetaka kuwahimiza wanawake wawe tayari kuripoti waume ambao wanawalazimisha kupashwa tohara,” alisema.
Wazee wa Njuri Ncheke wamekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ukeketaji tangu Aprili 1956 wakati baraza hilo lilipotangaza marufuku.