Habari Mseto

Msitii marufuku dhidi ya biashara ya mifugo, viongozi Tana River waambia wakazi

June 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

?Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wawili kutoka kaunti ya Tana River wamepinga marufuku iliyowekwa na maafisa wa afya ya mifugo dhidi ya biashara ya mifugo kufuatia mkurupuko wa Homa ya Rift Valley maeneo kadha katika kaunti hiyo.

Seneta wa Juma Wario na Mbunge wa Garsen Ali Wario waliwataka wakazi kupuuza mafuku hiyo wakisema ilitangazwa bila wao kushauriwa.

“Tunawashauri watu wetu kupuunza marufuku hiyo na waendelea kupeleka mifugo wao katika soko la Garsen, kama kawaida. Hii ni njama ya watu fulani wenye nia mbaya kuhujumu uchumi wa jamii za wafugaji ambayo tegemeo lao kuu ni mapato kutokana na biashara ya mifugo,” akasema Seneta Wario kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Ijumaa.

Mkurupuko wa Homa ya Rift Valley ulitokea katika eneo la kata ndogo ya Dhidh Ade katika eneo la Tana Delta. Watalaamu wanasema maradhi hayo ambayo husababisha na mbu yataendelea kuathiri maeneo mbalimbali hasa yale ambao bado yamelowa maji ambayo yanatoka katika mabwawa ya mradi wa kuzalisha stima wa Seven Forks.

“Watu wetu wamehangaishwa zaidi na mafuriko na hatungependa wazuiwe kuuza mifugo yao kama njia ya kujitafutia mapato ya kujikimu,” akasema Mbunge Wario.

Viongozi hao vile vile waliitaka kampuni ya kuzalisha umeme nchini KenGen kuwalipa ridhaa wakazi ambao wameathirika na maji kutoka kwa mabwawa yake.

Aidham, waliitaka serikali ya kitaifa kuwapa misaada wakazi ambao nyumba zao zimesombwa na maji hayo na sasa wanaishi ndani ya mahema.

“Tunataka KenGen ilipe ridhaa watu wetu ambao wamekuwa wakiendelea kuteseka baada ya makazi yao, mashamba yao na hata mifugo kusombwa na maji ambayo yalifunguliwa na kampuni hiyo kutoka kwa mabwawa yake ya kuzalisha yaliyoko sehemu ya juu ya mto Tana.,” akasema Seneta Wario.

Alisema takriban vijiji 30 katika eneo la Tana Delta vimezama ndani ya maji kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu sasa tangu mvua kubwa ilipoanza kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini.

“Zaidi ya watu 60,000 bado wanaishi ndani ya mahema yaliyochakaa huku wakikosa chakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi licha ya mvua kupungua. Mahangaiko haya yanaletwa na maji ambayo yalifunguliwa na kampuni ya KenGen kutoka kwa mabwawa yao,” akasema Bw Ali Wario.

Mbunge huyo aliitaka serikali kusambaza chakula cha misaada, dawa na malazi kwa watu hao, akisema Shirika la Msalaba Mwekundu (KRC) limelemewa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotaka msaada kutoka kwake.