Habari MsetoSiasa

Msomi ataka ushirikiano Pwani

February 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

WACHIRA MWANGI na WINNIE ATIENO

WAISLAMU katika eneo la Pwani wamehimizwa kuweka kando tofauti zao na kushirikiana kukabiliana na changamoto zinazowakumba.

Katibu mteule wa Utafiti katika wizara ya Kilimo, Profesa Hamadi Boga, alisema japokuwa eneo la Pwani lina matatizo mengi, viongozi wake wameshindwa kuyatatua kwa kukosa ushirikiano.

“Pwani tuko na changamoto za matumizi ya mihadarati, ukosefu wa elimu na misimamo mikali ya kidini. Haya ndiyo mambo ambayo twapaswa kushirikiana na kuyakabili kwa msimamo mmoja” akasema.

Naibu Chansela huyo wa Chuo Kikuu cha Taita Tateva ambaye amependekezwa kuongoza utafiti katika wizara ya Kilimo, alisema ni umoja tu utakaowasaidia watu wa Pwani.

Alikuwa akizungumza wakati wa hafla maalum katika uwanja wa Serani mjini Mombasa Ijumaa usiku, akiandamana na mfanyabiashara maarufu Bw Mohamed Jaffer.

Mfanyabiashara huyo aliwashauri watu wa Pwani kuwa wakakamavu na kujitolea kufanya kazi, na kuacha tabia ya ‘omba omba’ kwa wanasiasa.
Alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kuhakikisha uwanja wa Serani unapata hatimiliki baada ya miaka 35.

“Nimepigania hatimiliki ya ardhi hii kwa miaka 35. Kwanza nilienda kwa rais mstaafu Daniel Moi kumrai atupatie hati miliki lakini sikupata. Nikaenda kwa mrithi wake Mwai Kibaki na Raila Odinga lakini sikupata,” akaelezea umma.