Mswada bungeni kupunguza miaka ya kitambulisho hadi 16
Na SAMUEL OWINO
MBUNGE Maalum Gideon Keter ameandaa mswada ambao unaopendekeza serikali ipunguze miaka ya kupata kitambulisho cha kitaifa kutoka 18 hadi 16.
Mbunge huyo anataka sheria ya usajili wa watu kubadilishwa ili wanafunzi wa sekondari wawe wakipata kitambulisho kabla ya kumaliza shule.
Bw Keter alisema mswada huo uko tayari na atauwasilisha kwa karani wa bunge wiki hii.
Kwa sasa bunge liko kwenye likizo hadi Oktoba 2, wakati mswada huo utapangiwa kuangaziwa kwenye vikao vya bunge.
Kulingana na sheria ya usajili wa watu, vijana wanafaa kupewa kitambulisho cha kitaifa wakifikisha miaka 18, huku kila mtu akihitajika kujiwasilisha katika afisi za usajili siku 90 baada ya kufikisha umri huo.
Lakini hoja ya mbunge huyo inaibua mjadala ikiwa mtoto wa miaka 16 ataruhusiwa kupiga kura, kuingia katika ndoa ama kupata leseni ya kuendesha gari.
“Vijana wengi humaliza elimu ya shule za upili ama kupitisha miaka 18 bila vitambulisho na hii huleta changamoto kwa wengi wanapotafuta huduma,” akasema Bw Keter.
Mbunge huyo anahoji kuwa mchakato wa kupata kitambulisho nchini ni mrefu, ambao unaweza kuchukua hadi miaka miwili, hivyo akitaka watoto kutuma maombi ya kitambulisho wakiwa na miaka 16 ndipo wanapofikisha miaka 18 kinakuwa tayari.
“Kitambulisho ni nakala ambayo vijana wanafaa kupata kabla ya kumaliza shule ya upili, kwani wengi wanapatana na matatizo kwa kukosa nakala hiyo,” akasema.