• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mswada wapendekeza wanaotumia simu kucheza kamari wafungwe jela miaka miwili ama kulipa faini Sh2m

Mswada wapendekeza wanaotumia simu kucheza kamari wafungwe jela miaka miwili ama kulipa faini Sh2m

Na PETER MBURU

HUENDA maelfu ya Wakenya wanaotumia simu zao kucheza kamari mitandaoni kwa kubashiri matokeo ya michezo wakafungiwa huduma hizo ikiwa mswada ambao umewasilishwa bungeni utaidhinishwa kuwa sheria.

Kulingana na mswada huo, itakuwa hatia kucheza kamari kwa simu, na atakayepatikana akifanya hivyo atatozwa faini ya Sh2 milioni, ama kufungwa miaka miwili jela.

Ikiwa ni kampuni ambayo itakuwa ikichezesha kamari kwa simu, faini hiyo itapanda hadi Sh50 milioni, mswada huo kuhusu Kamari unasema.

Ni mswada ambao unapendekezwa kama mbinu ya kupunguza uchezaji kamari nchini, hasa miongoni mwa vijana.

Mswada huo unapendekeza utumiaji wa simu na vifaa vingine vya mawasiliano kucheza Kamari kudhibitiwa, katika uchumi ambapo huduma kama za MPESA zinawaruhusu watumizi wake kucheza michezo hiyo, bila kuwa na akaunti za benki.

Mswada huo unalenga kupunguza mzigo wa kamari kwa vijana wasio na kazi, ambao wanakisiwa kutumia hadi Sh5000 kucheza kamari kila mwezi.

“Mtu akiwa Kenya hawezi kutumia mfumo wa mawasiliano kwa ajili ya kucheza michezo kwenye mitandao, inayohusisha kamari, ya bahati nasibu, ya casino ama mingine ya kimitandao,” sehemu ya mswada huo inasema.

Aidha, sheria hiyo inataka kuharamisha utumiaji wa sava zilizoko nje ya nchi kwa michezo ya mitandaoni.

“Mamlaka ya Mawasiliano itahakikisha kuwa hakuna wahudumu kutoka mataifa mengine wanaotoa huduma za michezo watahudumu Kenya,” mswada unasema.

Sekta ya kamari nchini imekua kwa miaka mitano iliyopita, kufikia Sh200 bilioni, kutoka Sh2 bilioni, habari za serikali zinasema.

Wakenya wengi wamekuwa wakitumia simu kucheza Kamari mitandaoni.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Anawainua wazazi wanaolea peke yao

Wanyama aandalia Harambee Stars dhifa ya mlo wa jioni...

adminleo