Habari Mseto

Mtafaruku Rift Valley kuhusu mrithi wa Moi

November 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ONYANGO K’ONYANGO

MVUTANO mpya umeibuka kati ya kundi la wanasiasa eneo la Rift Valley wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto na wale wa Kiongozi wa Kanu Gideon Moi, kuhusu anayefaa kukabidhiwa nafasi ya kuwa kinara wa jamii hiyo.

Nafasi hiyo ilibaki wazi baada ya kuwa rais Mzee Daniel arap Moi kufariki Februari.

Chama cha Kanu kimemsuta Dkt Ruto kikidai anaendeleza njama ya kuwatumia baadhi ya wanachama wa baraza la wazee jamii ya Kalenjin, Myoot, kumtenga kiongozi wao aliye pia Seneta wa Baringo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Nick Salat kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumatatu alidai, Dkt Ruto anawatumia wazee kutoa madai yasiyo na msingi kuhusu uongozi wa jamii.

“Ulikuwa ni wajibu wa familia kufanya hiyo lakini hakuna sherehe iliyofanyika kumpokeza mtu yeyote vyombo hivyo vya uongozi. Hauwezi kusubiri hadi Mzee afariki kisha uanze kudai umepokezwa nafasi ya uongozi, kutoka wapi?” akauliza.

Baraza la Wazee wa Tugen lilirejeshea wenzao wa Nandi, zana za uongozi ambazo marehemu Mzee Moi alikabidhiwa mnamo 1955.

Myoot ni baraza kuu la wazee kutoka makabila madogo 10 ya jamii kubwa za Kalenjin kama vile Nandi, Kipsigis, Tugen, Marakwet, Keiyo, Pokot, Sabaot, Cherangany, Ogiek na Terik. Maamuzi ya baraza hilo huheshimiwa na mabaraza mengine ya wazee kutoka jamii zingine ndogo.

Baraza la Wazee wa Tugen likiongozwa na Kasisi Wilson Kibet Sambu lilisema, ingawa Seneta Moi ni Mtugen, wazee hawawezi kumkabidhi mamlaka ya uongozi ambayo babake alipewa kwa sababu vyombo vya uongozi vilitoka kwa wazee wa Nandi. Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima virudishwe.

Bw Benjamin Kitur ambaye ni mwenyekiti wa Myoot na Baraza la Wazee wa Nandi, Kaburow, alisema ataongoza mkutano wa baraza hilo (Myoot) hivi karibuni kuanzisha mchakato wa kumtaja msemaji wa jamii ya Kalenjin. Alifafanua kuwa hawatashawishiwa na wanasiasa.

Kulingana na Mbunge wa Aldai Cornelly Serem, mwandani wa Dkt Ruto, Naibu huyo wa Rais alitawazwa msemaji wa jamii ya Kalenjin mwongo mmoja uliopita.

“Ruto ndiye msemaji wa Rift Valley kwa sababu alitawazwa mnamo 2006 wakati Mzee Moi bado alikuwa hai. Tunajiandaa ili wazee wambariki rasmi na hadharani baada ya janga la corona kudhibitiwa,” akasema Bw Serem.

Ubabe wa kisiasa Rift Valley

Dkt Ruto amekuwa akishindana na Seneta Moi kuhusu ubabe wa kisiasa katika eneo la Rift Valley hali ambayo imezua mgawanyiko katika jamii ya Wakalenjin. Kila kambi imekuwa ikilaumu nyingine kwa kuijuhumu kwa nia ya kuendeleza masilahi finyu ya wachache badala ya jamii nzima ya Wakalenjin.

Hata hivyo, Bw Salat ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Dkt Ruto, alisema chama cha Kanu hakitayumbishwa na siasa hizo kiasi cha kusitisha juhudi zake za kujijenga upya kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema wakati huu, Kanu inamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika azma yake ya kutimiza ajenda zake za maendeleo na mpango wa kuunganisha taifa hili.

“Siasa zetu za mashinani sio muhimu kuliko mustakabali wa Kenya. Mustakabali huo hautayumbishwa na kile kilichopeanwa na kisichopeanwa. Kilicho muhimu ni kule ambako tunaenda kama taifa,” Bw Salat akasema.