Mtahiniwa wa KCSE atisha kuwaua Rais Kenyatta na Aden Duale
Na MANASE OTSIALO
MAAFISA wa polisi wanamzuilia mtahiniwa wa Kidato cha Nne kutoka Mandera na huenda wakamshtaki kuhusiana na makosa ya uhaini ikiwa wachunguzi hao wataweza kuthibitisha madai dhidi yake.
Ahmed Ali Abdi Adan, ambaye alikuwa miongoni mwa watahiniwa wa KCSE mwaka huu katika Shule ya Upili ya Elimu Bora mjini Mandera atajua ikiwa polisi wataendelea kumzuilia kwa siku saba kwa lengo la kumaliza uchunguzi Jumatatu.
Inadaiwa kuwa Adan, 19, aliwatumia ujumbe Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa wengi Bungeni Adan Duale na kuwatisha katika karatasi la majibu ya mtihani wa Kiingereza.
Aliwatishia kuwaua siku ambayo hakutaja katika ujumbe huo. Maafisa wa Baraza la Mtihani nchini (KNEC), Nairobi, walipata ujumbe huo walipokuwa wakiainisha makaratasi ya majibu ili kuanza kusahihisha Jumatatu.
“Tunaomba siku saba kumzuilia mshukiwa ili kukamilisha uchunguzi wetu kuhusiana na suala hilo kabla ya kumshtaki,” ilisema taarifa ya polisi.
Bw Allen Muluma, wakili wa serikali alisema madai dhidi ya mwanafunzi huyo yalikuwa ya uhaini.
Ili kujua aliyetuma ujumbe huo kwa Rais na Bw Duale, maafisa wa kusimamia mtihani walitumia nambari aliyosajiliwa nayo katika mtihani wa KCSE.
“Maafisa walifuatilia nambari ya usajili ya mtahiniwa ambayo iliwaelekeza hadi Shule ya Mseto ya Elimu Bora, Kaunti ya Mandera,” taarifa hiyo imesema.
Mwanafunzi mwingine na maafisa wawili wa mtihani kutoka shule hiyo ambayo ni ya kibinafsi wanakabiliwa na mashtaka ya kudanganya katika mtihani huo wa kitaifa katika Mahakama ya Mandera.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mandera, Dancun Mtai atatoa hukumu ikiwa atawaruhusu maafisa wa polisi kuendelea kumzuilia kwa siku saba Jumatatu.
Alielekeza maafisa hao kumpeleka mtahiniwa huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mandera kuchunguzwa hali ya kiakili kabla ya kutoa hukumu yake.
Ikiwa atashtakiwa kwa kosa la uhaini, Adan atakuwa amevunja rekodi iliyowekwa na watahiniwa wa Shule ya Wavulana ya Ambira ambao waliwatusi maafisa wa serikali.
Mnamo Novemba 26, Rais Kenyatta aliapa kukabiliana na wanafunzi wanaokosa heshima kwa watu wazima.