Habari Mseto

Mto Tana waanza kumeza shule na kuibua wasiwasi

May 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA STEPHEN ODUOR

HOFU imetanda kuhusu hatima ya wanafunzi karibu 1,200 wa shule iliyo eneobunge la Galole, Kaunti ya Tana River, ambayo inaendelea kuharibiwa na Mto Tana kila kukicha.

Shule ya Msingi ya Makere, kwa sasa iko chini ya mita 20 kutoka Mto Tana ambao umekuwa ukifurika baada ya mvua kubwa kushuhudiwa maeneo ya bara hivi majuzi.

Tangi la maji, jiko, nusu ya uzio wa shule, uwanja wa soka na ofisi ya chifu zimesombwa na maji mtoni tayari.

Darasa la chekechea liko umbali wa mita 14 tu kutoka mto huo ambao unameza karibu mita 10 za shule kila siku, wakati Madarasa 13 na jengo la utawala linalochukua robo iliyobaki ya ekari zinasimama umbali wa mita 30 tu.

Wakazi wanaona kuwa miundo iliyobaki inaweza kusombwa ndani ya wiki, kama Mto Tana utaendelea kufurika jinsi ilivyo kwa sasa.

“Mto huo ulikuwa umbali wa mita 300 kutoka shuleni, leo umemeza zaidi ya ekari moja ya shule na kila siku mchana na usiku unachukua zaidi,” alisema Komora Shushe, Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo.

Bw Shushe anahofia kwamba shule hiyo itasombwa na maji katika muda wa siku tatu zijazo, hivyo basi si salama kwa watoto kuripoti leo wakati shule zitakapofunguliwa kitaifa.

Kila saa, mto unapopanuka, shule inapungua kwa ukubwa.

Mwanajuma Guyo, makamu mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo anabainisha kuwa ardhi hiyo inaendelea kunyonya maji ya Mto Tana hivyo kuwa hatari kwa watoto.

“Jikoni lilikuwa hapa jana, tulipoamka leo halipo, kuna haja ya kutafuta uwanja mpya kwa ajili ya shule mpya, na tunatumai serikali itazingatia hili,” alisema.

Wazazi kwa upande mwingine wameazimia kuwaweka watoto wao nyumbani kwa muhula huu hadi wizara ya elimu itakaposhughulikia masaibu yao.

Wamesisitiza kuwa hatari inayowakabili watoto wanaporipoti shuleni huenda ikasababisha kupoteza maisha.

“Hatuwezi kuhatarisha, hiyo si shule tena, ni mtego wa kifo. Serikali ambayo imetangaza kufunguliwa kwa shule inapaswa kutuonyesha watoto wetu watakwenda kujifunza wapi kwa muhula huu,” alisema.

Mashirika ya kijamii ya Tana River yameiomba serikali kuingilia kati hali iliyopo katika Kaunti ya Tana River.

Kulingana na watetezi hao, hali katika shule nyingi ni mbaya, na haitafaa kwa watoto kurudi shuleni.

“Tunazungumza kuhusu wanafunzi 1,200 katika shule moja na tuna zaidi ya shule 15 zinazokabiliwa na tatizo hilo hilo, haziwezi kukaliwa na watu. Wizara inapaswa kufanya kitu kwa ajili ya watoto hawa,” alisema Mwenyekiti wa John Dhadho.

Hata hivyo, serikali ilipotangaza shule zifunguliwe leo, ilisema kuna baadhi ya kaunti ambapo shule hazitafunguliwa kwa vile bado kuna hatari ya mafuriko.

Kamishna wa Kaunti ya Tana River, Bw David Koskei, hata hivyo alisema kuwa watoto kutoka shule zilizoathiriwa na mafuriko watahifadhiwa na shule jirani, huku katika maeneo mengine serikali itaweka mahema.

Wakati huo huo, hatima ya watoto kutoka Lamu wanaofaa kusafiri hadi kaunti za nje kwa masomo bado haijulikani baada ya barabara kuu kufurika katika eneo la Gamba.

Barabara hiyo pia imefurika kwa maji kutoka Mto Tana.