Mtoto aliyefia kwenye mtaro Taveta azikwa familia ikiendelea kulilia haki
MTOTO wa miaka saba, aliyefariki Alhamisi iliyopita katika mtaro wa mkondo wa maji uliochimbwa kusambaza maji kwa shamba la Kisima ambalo linahusishwa na Rais William Ruto, amezikwa huku familia ikiendelea kulilia haki.
Mtoto huyo Daniel Kioko ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Grogan katika eneo la Mata Chini, Taveta, Kaunti ya Taita Taveta, alizikwa Ijumaa huku kukiwa na mwito wa uwajibikaji na hatua za usalama ili kuepuka maafa zaidi.
Waombolezaji walikosoa usimamizi wa shamba hilo kwa kuchelewa kushughulikia maswala ya usalama yaliyoibuliwa na wanakijiji hao ili kuzuia majanga ya aina hiyo.
Wakiongea wakati wa ibada ya mazishi, waombolezaji walitaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuhakikisha janga kama hilo halitokei tena wakisisitiza kuwa ipo haja ya hatua za haraka kuchukuliwa kuweka ua kwenye mtaro huo.
“Hii si mara ya kwanza tunazika mtoto kwa kufa katika ya mkondo huu. Tunataka usimamizi wa shamba kuchukua hatua za haraka kuzuia vifo na majeraha. Hatutakubali uzembe wa aina hii tena,” alisema mjombake mtoto huyo Bw John Kyallo.