• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Mtoto wa miaka 9 aokolewa kuolewa na mwanamume wa miaka 30

Mtoto wa miaka 9 aokolewa kuolewa na mwanamume wa miaka 30

Na STANLEY NGOTHO

MTOTO wa kike wa miaka tisa, mwishoni mwa wiki aliokolewa kabla ya kuozwa kwa mwanamume wa miaka 30 katika kijiji cha Ilmarba, Kaunti ya Kajiado.

Chifu wa eneo hilo, Bw Felix Maitei, aliwaongoza machifu wenzake na maafisa wa watoto hadi nyumba ambamo mtoto huyo alikuwa akiozwa.

Msichana huyo wa darasa la tatu kwanza alikeketwa ili kumtayarisha kuolewa na mwanaume ambaye wazazi wake walikuwa wamemchagulia.

Waokoaji walipofika walipata sherehe za harusi zikiendelea.

Habari zilisema jamaa wa mtoto huyo walikuwa tayari wamepokea ng’ombe sita pamoja na mali nyingine za mahari.

“Sherehe hiyo ya kumuoza msichana kwa mwanaume huyo ilikuwa ikiendelea tulipofika. Wazazi wake walijaribu kutuzuia kumuokoa lakini tuliwazidi nguvu,” alisema Bw Maitei.

Mtoto huyo baadaye alijiunga na wasichana wengine ambao wameokolewa kutokana na ndoa za mapema katika eneo hilo.

Mshirikishi shirika la haki za watoto, Kasisi Haron Ororuma, ambaye ni kati ya wale waliomuokoa mtoto huyo, alitaja kisa hicho kuwa cha unyama.

Naibu kamanda wa polisi katika Kaunti ya Kajiado, Charles Wambugu alisema maafisa wanawasaka walioendeleza shughuli hiyo.

“Wakati wa kuwaoza wasichana na kuwafanyisha vitendo vya tohara umepita. Ni vyema watu wa jamii ya Maasai wapewe mafunzo kuhusu haki za watoto na hatari ya kuwaoza mapema,” akasema Bw Wambugu.

Kutokana na kampeni ya kupiga vita utamaduni huo, wale ambao bado wanashiriki siku hizi wanaendesha shughuli hiyo usiku ili wasikamatwe.

You can share this post!

Raila akataa kutoa tiketi ya moja kwa moja Kibra

Uhuru akaa ngumu kuhusu marufuku ya kampuni za kamari

adminleo