Mucheru ashtua kwa kurefusha uanachama wa marehemu bodi ya KFCB
Na MARY WANGARI
WAZIRI wa Teknolojia ya Habari na Mawasilino (ICT) Joe Mucheru aliyekuwa amerefusha uanachama wa marehemu Robert Kochalle katika bodi ya Bodi ya Kitaifa ya Filamu Nchini (KFCB), sasa amteua mjane Charity Kochalle.
Hii ni baada ya Wakenya na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuonyesha ghadhabu kwa Bw Mucheru aliamua kumteua mjane wa marehemu.
Ni hatua ambayo ilionekana kuwakera baadhi ya Wakenya na watumiaji mitandao ya kijamii hata zaidi.
Bw Mucheru alijipata pabaya ambapo kupitia notisi rasmi iliyochapishwa gazetini mnamo Alhamisi, Oktoba 17, alimteua tena marehemu aliyeaga dunia mnamo Mei 2018, kuhudumu katika KFCB kwa miaka mingine mitatu.
“Kuambatana na mamlaka katika Kipengele 11A (e) cha Sheria kuhusu Michezo ya Filamu na Jukwaa, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia, anawateua tena Gathoni Kung’u, Robert Kochalle, Nereah Alouch Okanga, kama wanachama wa Bodi ya Kitaifa ya Filamu Nchini kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Octoba 21, 2019,” ilisema notisi hiyo.
Bw Kochella alikuwa mwanachama wa KFCB hadi alipofariki katika hospitali ya Aga Khan.
Hatua hii ilizua ghadhabu miongoni mwa Wakenya na watuniaji wengine wa mitandao ya kijamii walioshangazwa na kiwango cha utepetevu katika shughuli muhimu kama hiyo.
Suala dogo
Katika hatua iliyoonekana kuwatonesha wananchi hata zaidi, Mkurugenzi wa KFCB Ezekiel Mutua alijitosa mtandaoni Ijumaa kumtetea Bw Mucheru akipuuzilia mbali kosa lake kama suala dogo lililofanywa kuwa kubwa
“Suala dogo limefanywa kuwa kubwa kupita kiasi. Bodi iliwasilisha notisi kwa Wizara kuhusu teuzi mpya na akachaguliwa tena kimakosa. Halikuwa kosa la Waziri Mucheru hata kidogo maadamu ujumbe huo ulianza wakati KFCB ilikuwa chini ya Wizara ya Michezo na Utamaduni,” alisema Dkt Mutua kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Hata hivyo, hatua ya Bw Mucheru kumteua mjane wake marehemu Kochalle imeonekana kuwatamausha baadhi ya watu huku wakijitosa mitandaoni wakishangaa ni kwa nini nafasi za umma nchini huwa zinarithishwa miongoni mwa familia za viongozi na wengine kuuliza iwapo hakuna Wakenya wengine wenye ujuzi wa kutosha.
Mtumiaji mmoja kwa jina Bobi alionekana kukasirishwa kwelikweli.
“Yani hiki ni kichaa kipi? Hakuna Wakenya wengine waliofuzu kando na familia ya marehemu Robert Kochalle? Ni ama mfu au mkewe,” alifoka Bobi.
Pia Village Elder naye alikuwa na maoni kama hayo ya kughasika.
“Karibu katika jamhuri hii ambapo kazi hurithishwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Robert Kochalle anarithiwa – kikazi – na mkewe katika uteuzi. Vijana Wakenya ni sherehe baada ya sherehe,” alisikitika Village Elder.
Vilevile kuna mwingine anajiita Mwananchi.
“Mara tu unapoingia serikalini utakuwa daima serikalini. Unafariki wanakuchagua tena, kisha mke au mumeo kisha watoto. Hizi hisa za serikali ziko wapi tununue pia,” alisema Mwananchi.