Mudavadi ameza ndoano ya UDA
RAIS William Ruto anaandaa mpango thabiti wa kuinua Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi baada ya kuibuka kuwa waziri huyo wa Masuala ya Kigeni yuko tayari kuunganisha chama chake cha Amani National Congress (ANC) na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
Hatua hiyo mpya, hata hivyo, huenda ikavuruga washirika wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, hasa kutoka eneo la Mlima Kenya.
UDA imepanga uchaguzi wake mashinani kati ya Aprili 26 na Agosti 2 na utafuatiwa na uchaguzi katika kaunti na kitaifa kufikia Desemba.
Taifa Leo imebaini kuwa Ruto ameanza shinikizo jipya kwa washirika wake katika Muungano wa Kenya Kwanza kuvunja vyama vyao na kujiunga na chake.
Bw Mudavadi, kulingana na duru za ndani, haoni tatizo kushawishi kikosi chake cha ANC kujiunga na UDA ili kuimarisha chama tawala kabla ya uchaguzi wa 2027, na kuimarisha mustakabali wake wa kisiasa siku zijazo.
Hata hivyo, hatua hii bado inaweza kukabiliwa na upinzani, hasa eneo la Magharibi, kwani viongozi wengine wanaiona kama ya kujiua kisiasa.
Ingawa Bw Mudavadi alibanduka kutoka wadhifa wake wa kiongozi wa chama cha ANC na kuachia usukani Gavana wa Lamu Issa Timamy baada ya kuteuliwa Mkuu wa Mawaziri anaweza kunufaika na mojawapo ya nafasi za Naibu Kiongozi wa Chama, nafasi ambayo itamweka kisiasa katika ngazi moja Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Kifungu cha 24 cha Katiba ya UDA kinaorodhesha viongozi 39 wa chama, ambapo kuna kiongozi mmoja wa chama na manaibu watatu.
Inatoa nyadhifa za Naibu Kiongozi wa Chama anayehusika na Sera na Mikakati, Naibu Kiongozi wa Chama anayehusika na Operesheni na Naibu Kiongozi wa Chama anayesimamia Mipango.
Hivi majuzi, Bw Mudavadi alidokeza kwamba kutakuwa na wimbi jingine la “tsunami ya kisiasa,” sawa na lile alilodokeza wakati wa kujiunga kwake na Rais Ruto kabla ya uchaguzi wa Agosti 2022.
Alipendekeza hatua mpya
Vile vile, alipendekeza hatua mpya aliyosema itakipa nguvu chama cha UDA.
“Nawataka wafuasi wengine wa ANC waelewe kuwa japo mimi si afisa wa chama leo, lakini kama mwanachama mwaminifu sharti niwaambie wazi kuwa sharti tulenge kuupa nguvu utawala wa Kenya Kwanza na kufanya kazi na UDA ambacho ni chama kikuu katika muungano huo. Pia tunapaswa kushiriki katika mijadala mingine kwa kina. Usiniulize ni mijadala ipi ya kina. Hilo litajibiwa siku nyingine. Tsunami nyingine inanukia,” Bw Mudavadi alidai.
Kiranja wa Wengi Boni Khalwale, ambaye pia ni Seneta wa Kakamega amewahi kudokeza waziwazi kuhusu uwezekano wa Bw Mudavadi kujiunga na UDA.
Inaonekana nyota ya Mudavadi inang’aa kwa kasi. Mara ya kwanza aliteuliwa Mkuu wa Mawaziri (PCS) na kisha akaongezewa wadhifa wenye ushawishi mkubwa wa Waziri wa Masuala ya Kigeni.
Aidha, Rais Ruto amewahi kuelezea waziwazi kuwa anamwamini Bw Mudavadi.
“Ndugu yangu Musalia Mudavadi, kuhusu masuala ya kidiplomasi, sote tunaafikiana kwamba yeye ni mwanadiplomasia bora. Ndiposa nikikosa nafasi ya kusafiri kuenda nje, mataifa mengi huniambia ni sawa nikimtuma Mudavadi. Atafanya kila kitu namna ambavyo ningefanya. Nakushukuru kwa moyo wako wa kujitolea katika majukumu yako,” Rais akasema juzi.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema kuwa Bw Mudavadi anajua kwamba ANC haiwezi kukabiliana na UDA kwenye uchaguzi.