Habari Mseto

Mukhisa Kitui atangaza nia ya kugombea urais

August 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WACHIRA MWANGI

KATIBU Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi amethibitisha nia yake ya kujiunga na kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Kituyi ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge wa Kimilili na Waziri, alidokeza kuwa atajitosa katika safari ya kuenda Ikulu baada ya muda wake wa kuhudumu katika shirika hilo la kimataifa kukamilika mwaka ujao.

Tangazo lake linaashiria kuwa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ambao pia wanakimezea mate kiti hicho watapata upinzani mkuu nyumbani ikizingatiwa kuwa Dkt Kituyi pia anatoka Magharibi ya Kenya.

Wanasiasa wengine wanaopania kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ni Naibu wake William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka.

“Kuhusu ikiwa nitawania urais wa Kenya au la, nimebuni kamati maalum ambayo inaendesha mazungumzo na marafiki kote nchini kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho,” akasema alipotembelea afisi ya Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda (KNCCI), tawi la Mombasa.

“Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa tunajiunga na kinyang’anyiro baada ya kukamilisha kazi katika ngazi ya kimataifa,” Dkt Kituyi akawaambia wanahabari alipokuwa akijibu swali kuhusu mustakabali wake katika siasa za Kenya.

Alisema Kenya inahitaji uongozi ambao unaweza kuifanya Kenya iwe na nafasi bora katika ngazi ya kibiashara ulimwenguni.

Kulingana na Dkt Kituyi, serikali inapasa kupiga jeki wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini huku ikiendeleza vita dhidi janga la corona badala ya suluhisho la kisiasa linalowafaidi watu wachache serikalini.

“Kinachohitajika nchini ni kukabili changamoto inayoisibu uchumi kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu. Tishio kubwa kwa demokrasia nchini ni pengo kati ya kile ambacho wanasiasa wanasema ni hisia za watu wa maeneo ya mashinani,” akasema.

Dkt Kituyi alikashifu siasa zinazohusishwa na Mpango wa Maridhiano (BBI) na mjadala kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti akisema hazina manufaa kwa mwananchi wa kawaida.

Kando na kuwa msomi na mwanasiasa, Katibu huyo mkuu UNCTAD ana tajiriba pana katika masuala ya utawala, biashara na diplomasia.

Dkt Kituyi, 64, alizaliwa katika kaunti ya Bungoma, Magharibi ya Kenya.

Alisomea taaluma ya sayansi ya siasa na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi na baadaye katika chuo kikuu cha Makerere ambako alifuzu mnamo 1982.

Alipata shahada ya uzamili mnamo 1986 kisha shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Bergen, Norway.